Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 2:12-25

1 Wafalme 2:12-25 NEN

Kwa hiyo Solomoni akaketi katika kiti cha ufalme cha baba yake Daudi, nao utawala wake ukaimarika sana. Basi Adoniya, mwana wa Hagithi, akaenda kwa Bathsheba, mama yake Solomoni. Bathsheba akamuuliza, “Je, umekuja kwa amani?” Akajibu, “Ndiyo, kwa amani.” Kisha akaongeza, “Ninalo jambo la kukuambia.” Akajibu, “Waweza kulisema.” Akasema, “Kama unavyojua, ufalme ulikuwa wangu. Israeli wote waliniangalia mimi kama mfalme wao. Lakini mambo yalibadilika, ufalme umekwenda kwa ndugu yangu, kwa maana umemjia kutoka kwa BWANA. Sasa ninalo ombi moja ninalokuomba. Usinikatalie.” Bathsheba akasema, “Waweza kuliomba.” Kwa hiyo akaendelea kusema, “Tafadhali mwombe Mfalme Solomoni, anipatie Abishagi, Mshunami, awe mke wangu; hatakukatalia wewe.” Bathsheba akamjibu, “Vema sana, nitazungumza na mfalme kwa ajili yako.” Bathsheba alipokwenda kwa Mfalme Solomoni kuzungumza naye kwa ajili ya Adoniya, mfalme alisimama kumlaki mama yake, akamwinamia na kuketi kwenye kiti chake cha ufalme. Akaamuru kiti cha ufalme kuletwa kwa ajili ya mama yake mfalme, naye akaketi mkono wake wa kuume. Bathsheba akamwambia mfalme, “Ninalo ombi moja dogo la kukuomba; usinikatalie.” Mfalme akajibu, “Omba, mama yangu; sitakukatalia.” Akasema, “Mruhusu Abishagi, Mshunami, aolewe na ndugu yako Adoniya.” Mfalme Solomoni akamjibu mama yake, “Kwa nini uombe Abishagi, Mshunami, kwa ajili ya Adoniya? Ungeweza pia kuomba ufalme kwa ajili yake, kwani yeye ni ndugu yangu mkubwa: naam, kwa ajili yake, na kwa kuhani Abiathari na Yoabu mwana wa Seruya!” Mfalme Solomoni akaapa kwa BWANA, akasema: “Mungu na aniulie mbali, tena bila huruma, ikiwa Adoniya hatalipa kwa uhai wake kwa ajili ya ombi hili! Basi sasa, hakika kama BWANA aishivyo, yeye ambaye ameniimarisha salama kwenye kiti cha ufalme cha Daudi baba yangu, naye amenipa ufalme wa kudumu kama alivyoahidi, Adoniya atauawa leo!” Hivyo Mfalme Solomoni akatoa amri kwa Benaya mwana wa Yehoyada, naye akampiga Adoniya akafa.