1 Wakorintho 16:13-24
1 Wakorintho 16:13-24 NEN
Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari. Fanyeni kila kitu katika upendo. Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio waliokuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi, mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii. Nilifurahi wakati Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa. Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu sana katika Bwana. Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu. Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kama mtu yeyote hampendi Bwana Yesu Kristo, na alaaniwe. Bwana wetu, njoo. Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi. Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Amen.