1 Wakorintho 16:13-24
1 Wakorintho 16:13-24 NENO
Kesheni; simameni imara katika imani; kuweni mashujaa na hodari. Fanyeni kila kitu katika upendo. Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio walikuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi, mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii. Nilifurahi Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu. Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa. Makundi ya waumini wa jimbo la Asia wanawasalimu. Akila na Prisila pamoja na kundi la waumini walioko nyumbani mwao wanawasalimu sana katika Bwana Isa. Ndugu wote walio hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu. Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kama mtu yeyote hampendi Bwana Isa Al-Masihi, na alaaniwe. Bwana wetu Isa, njoo. Neema ya Bwana Isa iwe nanyi. Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Al-Masihi Isa. Amen.