Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Nyakati 5

5
Wana wa Reubeni
1Wana wa Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli (yeye alikuwa mzaliwa wa kwanza, lakini kwa kuwa alikinajisi kitanda cha baba yake, haki zake za mzaliwa wa kwanza walipewa wana wa Yusufu mwana wa Israeli. Hivyo hakuorodheshwa kwenye orodha ya ukoo wao kulingana na haki yake ya kuzaliwa. 2Na ingawa Yuda alikuwa na nguvu zaidi ya ndugu zake wote, na mtawala alitoka kwake, haki za mzaliwa wa kwanza zilikuwa za Yusufu.) 3Wana wa Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli walikuwa:
Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.
4Wazao wa Yoeli walikuwa:
Shemaya mwanawe, Gogu mwanawe;
Shimei mwanawe, 5Mika mwanawe,
Reaya mwanawe, Baali mwanawe,
6na Beera mwanawe, ambaye Tiglath-Pileseri mfalme wa Ashuru alimchukua kwenda uhamishoni. Beera alikuwa kiongozi wa Wareubeni.
7Jamaa zao kulingana na koo zao, walioorodheshwa kwa koo zao kama ifuatavyo:
Yeieli aliyekuwa mkuu wao, Zekaria, 8Bela mwana wa Azazi, mwana wa Shema, mwana wa Yoeli.
Hao waliishi katika eneo lililoanzia Aroeri hadi Nebo na Baal-Meoni. 9Kwa upande wa mashariki walienea hadi pembeni mwa jangwa linaloenea hadi kwenye Mto Frati, kwa sababu mifugo yao ilikuwa imeongezeka huko Gileadi.
10Wakati wa utawala wa Mfalme Sauli, walipigana vita dhidi ya Wahagari, wakaanguka kwa mikono yao. Kisha wakaishi katika mahema ya Wahagari katika eneo lote la mashariki mwa Gileadi.
Wana wa Gadi
11Wagadi waliishi jirani nao katika nchi ya Bashani, hadi Saleka.
12Yoeli ndiye alikuwa mkuu wao, Shafamu wa pili, na wakafuata Yanai na Shafati, huko Bashani.
13Ndugu zao, kulingana na jamaa zao, walikuwa saba:
Mikaeli, Meshulamu, Sheba, Yorai, Yakani, Zia na Eberi.
14Hao walikuwa wana wa Abihaili mwana wa Huri, mwana wa Yaroa, mwana wa Gileadi, mwana wa Mikaeli, mwana wa Yeshishai, mwana wa Yahdo, mwana wa Buzi.
15Ahi mwana wa Abdieli, mwana wa Guni, alikuwa kiongozi wa jamaa yao.
16Wagadi waliishi Gileadi, huko Bashani pamoja na vijiji vyake, na pia katika maeneo yote ya malisho ya Sharoni kote walikofika.
17Yote haya yaliwekwa katika kumbukumbu za ukoo wao wakati wa utawala wa Yothamu, mfalme wa Yuda na Yeroboamu mfalme wa Israeli.
18Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase walikuwa na wanaume elfu arobaini na nne mia saba na sitini (44,760) waliokuwa tayari kwenda vitani, wanaume wenye uwezo wa kutumia ngao na upanga, ambao wangeweza kutumia upinde, walioandaliwa kwa vita. 19Walipigana vita dhidi ya Wahagari, Yeturi, Nafishi na Nodabu. 20Walisaidiwa katika kupigana nao, Mungu akawatia Wahagari pamoja na wote walioungana nao mikononi mwao, kwa sababu walimlilia Mungu wakati wa vita. Alijibu maombi yao, kwa sababu walimtegemea. 21Walitwaa mifugo ya Wahagari: ngamia elfu hamsini, kondoo elfu mia mbili na hamsini, na punda elfu mbili. Pia wakateka watu elfu mia moja, 22na wengine wengi waliuawa kwa sababu vita vilikuwa ni vya Mungu. Nao waliendelea kuikalia nchi hiyo hadi wakati wa uhamisho.
Nusu ya Kabila la Manase
23Idadi ya nusu ya kabila la Manase walikuwa wengi sana, Wakakaa kuanzia Bashani hadi Baal-Hermoni, yaani Seniri (ndio Mlima Hermoni).
24Hawa walikuwa viongozi wa jamaa za kabila hilo: Eferi, Ishi, Elieli, Azrieli, Yeremia, Hodavia na Yadieli. Walikuwa askari shujaa, watu maarufu, viongozi wa jamaa zao. 25Lakini hawakuwa waaminifu kwa Mungu wa baba zao, nao wakafanya ukahaba kwa miungu ya mataifa, ambayo Mungu alikuwa ameyaangamiza mbele yao. 26Kwa hiyo Mungu wa Israeli akaiamsha roho ya Pulu, mfalme wa Ashuru (ambaye pia alijulikana kama Tiglath-Pileseri), ambaye aliwachukua Wareubeni, Wagadi na nusu ya kabila la Manase kwenda uhamishoni. Akawapeleka huko Hala, Habori, Hara na mto Gozani, ambako wamekaa hadi leo.

Iliyochaguliwa sasa

1 Nyakati 5: NENO

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia