1 Nyakati 21:1-13
1 Nyakati 21:1-13 NENO
Shetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu Waisraeli. Kwa hiyo, Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba hadi Dani. Kisha mniletee taarifa niweze kufahamu wako wangapi.” Yoabu akajibu, “Mwenyezi Mungu na aongeze jeshi lake mara mia na zaidi. Mfalme bwana wangu, kwani hawa wote si raia wa bwana wangu? Kwa nini bwana wangu unataka kufanya hivi? Kwa nini kuleta hatia juu ya Israeli?” Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu; kwa hiyo Yoabu akaondoka na kuzunguka Israeli yote, kisha akarudi Yerusalemu. Yoabu akamtolea Daudi idadi ya wapiganaji: Katika Israeli yote kulikuwa na watu milioni moja na elfu mia moja ambao wangeweza kutumia upanga, wakiwemo watu elfu mia nne sabini wa Yuda. Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli. Kisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.” Mwenyezi Mungu akamwambia Gadi, mwonaji wa Daudi, “Nenda ukamwambie Daudi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ” Kwa hiyo Gadi akamwendea Daudi akamwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Chagua: miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu ya kushindwa na adui zako, ukipatwa na panga zao; au siku tatu za upanga wa Mwenyezi Mungu: siku tatu za tauni katika nchi na malaika wa Mwenyezi Mungu akiangamiza kila mahali katika Israeli.’ Sasa basi, amua jinsi nitakavyomjibu yeye aliyenituma.” Daudi akamwambia Gadi, “Ninayo mahangaiko makubwa. Mimi na nianguke mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa maana rehema zake ni kuu mno, lakini usiniache niangukie mikononi mwa wanadamu.”