1 Nyakati 21
21
Daudi ahesabu wapiganaji
(2 Samweli 24:1-25)
1Shetani akainuka dhidi ya Israeli na kumshawishi Daudi ahesabu Waisraeli. 2Kwa hiyo, Daudi akamwambia Yoabu na majemadari wa jeshi, “Nendeni mkawahesabu Waisraeli kuanzia Beer-Sheba hadi Dani. Kisha mniletee taarifa niweze kufahamu wako wangapi.”
3Yoabu akajibu, “Mwenyezi Mungu na aongeze jeshi lake mara mia na zaidi. Mfalme bwana wangu, kwani hawa wote si raia wa bwana wangu? Kwa nini bwana wangu unataka kufanya hivi? Kwa nini kuleta hatia juu ya Israeli?”
4Hata hivyo, neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu; kwa hiyo Yoabu akaondoka na kuzunguka Israeli yote, kisha akarudi Yerusalemu. 5Yoabu akamtolea Daudi idadi ya wapiganaji: Katika Israeli yote kulikuwa na watu milioni moja na elfu mia moja ambao wangeweza kutumia upanga, wakiwemo watu elfu mia nne sabini wa Yuda.
6Lakini Yoabu hakuwahesabu Walawi na Wabenyamini, kwa sababu alichukizwa sana na amri ya mfalme. 7Amri hii ilikuwa mbaya machoni pa Mungu pia; hivyo akaiadhibu Israeli.
8Kisha Daudi akamwambia Mungu, “Nimetenda dhambi kubwa kwa kufanya jambo hili. Sasa, ninakusihi, ondoa hatia ya mtumishi wako. Nimefanya jambo la kipumbavu sana.”
9Mwenyezi Mungu akamwambia Gadi, mwonaji wa Daudi, 10“Nenda ukamwambie Daudi, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Ninakupa wewe uchaguzi wa mambo matatu. Nichagulie mojawapo nitakalotenda dhidi yako.’ ”
11Kwa hiyo Gadi akamwendea Daudi akamwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: ‘Chagua: 12miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu ya kushindwa na adui zako, ukipatwa na panga zao; au siku tatu za upanga wa Mwenyezi Mungu: siku tatu za tauni katika nchi na malaika wa Mwenyezi Mungu akiangamiza kila mahali katika Israeli.’ Sasa basi, amua jinsi nitakavyomjibu yeye aliyenituma.”
13Daudi akamwambia Gadi, “Ninayo mahangaiko makubwa. Mimi na nianguke mikononi mwa Mwenyezi Mungu, kwa maana rehema zake ni kuu mno, lakini usiniache niangukie mikononi mwa wanadamu.”
14Basi Mwenyezi Mungu akatuma tauni katika Israeli, na wanaume elfu sabini wa Israeli wakafa. 15Mungu akapeleka malaika kuangamiza Yerusalemu. Lakini malaika alipokuwa akifanya hivyo, Mwenyezi Mungu akaona na akahuzunika kwa sababu ya maafa, akamwambia yule malaika aliyekuwa anaangamiza watu, “Yatosha! Rudisha mkono wako.” Wakati huo malaika wa Mwenyezi Mungu alikuwa amesimama katika sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna#21:15 au Ornani kwa Kiebrania Myebusi.
16Daudi akayainua macho yake, akamwona huyo malaika wa Mwenyezi Mungu akiwa amesimama katikati ya mbingu na dunia, naye ameunyoosha upanga wake juu ya Yerusalemu tayari kuangamiza. Kisha Daudi na wazee, waliokuwa wamevaa gunia, wakaanguka kifudifudi.
17Daudi akamwambia Mungu, “Je, si mimi ndiye niliyeamuru watu wahesabiwe? Mimi ndiye niliyetenda dhambi na kukosa. Hawa ni kondoo tu. Wamefanya nini? Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu, mkono wako na uwe juu yangu na jamaa yangu, lakini usiache tauni hii iendelee juu ya watu wako.”
Daudi ajenga madhabahu
18Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akamwamuru Gadi amwambie Daudi apande na kumjengea Mwenyezi Mungu madhabahu kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Arauna Myebusi. 19Kwa hiyo Daudi akakwea, akalitii lile neno ambalo Gadi alikuwa amelisema katika jina la Mwenyezi Mungu.
20Arauna alipokuwa akipura ngano, akageuka, akamwona yule malaika. Wanawe wanne waliokuwa pamoja naye wakajificha. 21Kisha Daudi akakaribia, Arauna alipotazama na kumwona, akaondoka kwenye uwanja wa kupuria nafaka akamsujudia Daudi, uso wake ukagusa chini.
22Daudi akamwambia Arauna, “Nipatie huu uwanja wako wa kupuria nafaka, niweze kujenga madhabahu ya Mwenyezi Mungu, ili tauni ipate kukomeshwa katika watu. Niuzie kwa bei yake kamili.”
23Arauna akamwambia Daudi, “Uchukue huo uwanja. Mfalme bwana wangu na afanye lolote analopenda. Tazama, nitatoa maksai kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, vifaa vya kupuria kuwa kuni, pamoja na ngano kwa ajili ya dhabihu ya nafaka. Natoa hivi vyote.”
24Lakini Mfalme Daudi akamjibu Arauna, “La hasha! Lakini ninasisitiza kwamba nitalipa bei yake kamili. Sitachukua kilicho chako kwa ajili ya Mwenyezi Mungu au kutoa sadaka ya kuteketezwa isiyonigharimu chochote.”
25Basi Daudi akamlipa Arauna shekeli mia sita#21:25 Shekeli 600 ni sawa na kilo 7. za dhahabu kwa ajili ya ule uwanja. 26Kisha Daudi akamjengea Mwenyezi Mungu madhabahu mahali hapo, na kutoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Akamwita Mwenyezi Mungu naye Mwenyezi Mungu akajibu maombi yake kwa moto kutoka mbinguni juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
27Kisha Mwenyezi Mungu akanena na yule malaika, naye akarudisha upanga wake katika ala yake. 28Wakati huo, Daudi alipoona kwamba Mwenyezi Mungu amemjibu kule kwenye uwanja wa kupuria nafaka wa Arauna Myebusi, akatoa dhabihu huko. 29Maskani ya Mwenyezi Mungu ambayo Musa aliitengeneza kule jangwani, pamoja na madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kwa wakati huo vilikuwa viko mahali pa juu pa kuabudia huko Gibeoni. 30Lakini Daudi hakuthubutu kuisogelea ili kumuuliza Mungu, kwa sababu aliuogopa upanga wa yule malaika wa Mwenyezi Mungu.
Iliyochaguliwa sasa
1 Nyakati 21: NENO
Kuonyesha
Shirikisha
Nakili

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.