1 Mambo ya Nyakati 21:1-13
1 Mambo ya Nyakati 21:1-13 SRUV
Tena shetani akasimama juu ya Israeli, akamshawishi Daudi kuwahesabu Waisraeli. Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao. Naye Yoabu akasema, BWANA na awaongeze watu wake mara mia hesabu yao ilivyo; lakini, bwana wangu mfalme, si wote watumishi wa bwana wangu? Mbona basi bwana wangu analitaka neno hili? Mbona alete hatia kwa Israeli? Lakini neno la mfalme likawa na nguvu juu ya Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akaenda zake, akapita kati ya Israeli wote, akafika Yerusalemu. Naye Yoabu akamtolea Daudi jumla ya hesabu ya watu. Na hao wote wa Israeli walikuwa watu milioni moja na laki moja, wenye kufuta panga; na wa Yuda watu elfu mia nne sabini (470,000), wenye kufuta panga. Lakini Lawi na Benyamini hakuwahesabu miongoni mwao; kwa sababu neno la mfalme limemchukiza Yoabu. Neno hilo likawa baya machoni pa Mungu; kwa hiyo akawapiga Israeli. Naye Daudi akamwambia Mungu, Nimekosa sana, kwa kuwa nimelifanya jambo hili; lakini sasa uuondolee mbali, nakusihi, uovu wa mtumishi wako; kwani nimefanya upumbavu kabisa. Naye BWANA akanena na Gadi, mwonaji wake Daudi, akisema, Nenda ukanene na Daudi, ukisema, BWANA asema hivi, Nakuwekea mambo matatu; katika haya ujichagulie moja, nikutendee hilo. Basi Gadi akamwendea Daudi, akamwambia, BWANA asema hivi, Jichagulie upendavyo; miaka mitatu ya njaa; au miezi mitatu kuangamia mbele ya adui zako, ukipatwa na upanga wa watesi wako; au siku tatu upanga wa BWANA, yaani tauni katika nchi, na malaika wa BWANA akiharibu kati ya mipaka yote ya Israeli. Haya basi ufikiri ni jawabu gani nimrudishie yeye aliyenituma. Naye Daudi akamwambia Gadi, Nimeingia katika mashaka sana; basi sasa na nianguke katika mkono wa BWANA; kwa kuwa rehema zake ni nyingi sana; wala nisianguke katika mkono wa wanadamu.