BibleProject | Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio / Sehemu ya 1 - LukaPrøve
Ufalme wa Yesu ni habari njema kwa wanaoteseka, na ni kwa wote wanaofahamu kuwa wanamhitaji Mungu. Ili kufafanua hili, Luka anatueleza kitendo cha Yesu kuhudhuria karamu za jioni ambako kulikuwa na wagonjwa na maskini waliopokea msamaha, uponyaji na ukarimu wake. Kwa upande mwingine, Yesu pia anahudhuria karamu za jioni ambako kulikuwa na viongozi wa dini waliokataa mafundisho yake na kukosoa mbinu zake. Hawafahamu Ufalme wa Mungu unahusu nini, hivyo anawapa mfano. Alisimulia kama ifuatavyo.
Kulikuwepo na baba aliyekuwa na wana wawili. Mwana wa kwanza ni mwadilifu na anamheshimu baba yake, lakini yule mdogo amepotoka. Anachukua urithi wake mapema, anakwenda nchi ya mbali na kuutumia kwa uasherati na anasa. Baadaye njaa kuu inaingia nchi ile na mali yake inakwisha, naye anapata kazi ya kuwalisha nguruwe. Siku moja anapatwa na njaa kali mpaka yuko tayari kula chakula cha nguruwe, na hapo ndipo akawaza kuwa maisha yangekuwa bora angelikuwa mtumishi wa baba yake. Hivyo anaondoka na kurejea nyumbani, huku akifanya mazoezi ya jinsi atakavyoomba msamaha. Anapokuwa angali mbali, baba yake anamwona na anajawa na furaha. Mwanaye yu hai! Hajaangamizwa na njaa! Baba anamwendea mbio na anamkumbatia na kumbusu. Mwana anaanza kwa kusema, “Baba, sistahili kuitwa mwanao. Nifanye mmoja wa watumishi wako...” Lakini kabla hajamaliza kunena, baba anawatuma watumishi wake wamletee mwanawe vazi lililo bora wamvike, viatu vipya na pete nzuri. Wanapaswa kuandaa karamu kuu kwa sababu ni wakati wa kusherehekea kurejea kwa mwana. Karamu inapoanza, yule ndugu mkubwa anarejea akiwa ametoka kufanya kazi ngumu na anapofika anagundua kuwa muziki na vyakula vimeandaliwa kwa ajili ya ndugu yake mpotevu. Anakasirika na anakataa kuingia kwenye karamu. Baba anamkuta mwanawe wa kwanza nje na anamwambia, “mwanangu, tayari wewe ni sehemu ya familia yetu. Vyote nilivyo navyo ni vyako. Lakini ilitupasa tusherehekee kurejea kwa ndugu yako. Alikuwa amepotea lakini sasa amerejea. Alikuwa amekufa, lakini sasa yu hai.”
Kwenye simulizi hii, Yesu anawalinganisha viongozi wa kidini na yule mwana wa kwanza. Yesu anaona jinsi viongozi wa dini wanaghadhabishwa na anavyowapokea wenye dhambi, lakini Yesu angependa viongozi hawa wawachukulie wenye dhambi jinsi yeye anavyowachukulia. Wenye dhambi wanarejea kwa baba yao. Wana uzima! Wema wa Mungu unawatosha watu wote. Vyote alivyo navyo ni vya wale anaowaita wana wake.
Kinachohitajika tu ili kufurahia Ufalme wake ni kuupokea kwa unyenyekevu. Soma, Tafakari kisha Ujibu:
•Je, maisha yako yanafanana vipi na ya yule mwana wa kwanza na yule wa pili kwenye fumbo la Yesu?
•Tazama jinsi mwana wa pili alivyoondoka nyumbani kwa baba yake lakini akabadili nia yake mambo yalipokuwa magumu. Je, hali ngumu imewahi kukusaidia kumrudia Mungu Baba? Je, unajifunza yepi kutokana na jinsi baba anavyomkaribisha mwanawe wa pili (soma 15:20-24)?
•Hebu fikiria kuhusu hasira ya yule mwana wa kwanza kwenye simulizi (soma 15:28-30). Je, umewahi kutofurahia mtu alipotunukiwa kitu asichostahili? Ikiwa umewahi, unachukuliaje jibu la baba kwa mwanawe wa kwanza (soma 15:31-32)?
•Kusoma na kutafakari kwako kukuchochee kuomba. Zungumza na Mungu kuhusu jinsi fadhili zake ni za ajabu, kiri kuhusu udhaifu wako wa kuwapokea wengine kwa ukarimu na uombe unachohitaji ili uweze kuwa mwenye fadhili.
Om denne planen
Shirika la BibleProject liliandaa mwongozo wa Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio Sehemu ya 1 kuwahimiza watu binafsi, vikundi vidogo na familia kusoma kitabu chote cha Luka kwa siku 20. Mwongozo huu unajumuisha video za katuni, muhtasari wa uchambuzi na maswali ya kutafakari ili kuwasaidia wahusika kumfahamu Yesu na kufuatilia mtiririko wa mawazo ya Luka pamoja na kuyaelewa mafunzo yake.
More