Yohana 4

4
Isa Azungumza Na Mwanamke Msamaria
1 Mafarisayo#4:1 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakasikia kwamba Isa alikuwa anapata na kubatiza wanafunzi wengi zaidi kuliko Yahya, 2 ingawa kwa kweli si Isa mwenyewe aliyekuwa akibatiza, ila ni wanafunzi wake. 3 Bwana Isa alipojua mambo haya, aliondoka Uyahudi akarudi tena Galilaya.
4 Wakati huo ilimlazimu apitie Samaria. 5 Akafika kwenye mji mmoja wa Samaria uitwao Sikari, karibu na lile shamba ambalo Yakobo alimpa mwanawe Yusufu. 6Huko ndiko kulikokuwa na kile kisima cha Yakobo. Naye Isa alikuwa amechoka kwa kuwa alikuwa ametoka safarini. Akaketi karibu na hicho kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
7 Mwanamke mmoja Msamaria akaja kuteka maji, Isa akamwambia, “Naomba maji ninywe.” 8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
9 Yule mwanamke Msamaria akamjibu, “Wewe ni Myahudi na mimi ni Msamaria. Yawezekanaje uniombe nikupe maji ya kunywa?” Wayahudi walikuwa hawashirikiani kabisa na Wasamaria.
10 Isa akajibu akamwambia, “Kama ungelijua karama ya Mungu, naye ni nani anayekuambia, Nipe maji ninywe, wewe ungelimwomba yeye, naye angelikupa maji yaliyo hai.”
11Yule mwanamke akamjibu, “Bwana,#4:11 Wale ambao hawakumfahamu Isa kuwa Masihi walimwita “Bwana” kwa heshima ya kawaida. wewe huna chombo cha kutekea maji na kisima hiki ni kirefu. Hayo maji ya uzima utayapata wapi? 12 Kwani wewe ni mkuu kuliko baba yetu Yakobo ambaye alitupatia kisima hiki, ambacho yeye pamoja na watoto wake na mifugo yake walikitumia?”
13 Isa akamjibu, “Kila mtu anayekunywa maji ya kisima hiki, ataona kiu tena. 14 Lakini yeyote anywaye maji nitakayompa, hataona kiu kamwe. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji yakibubujika uzima wa milele.”
15 Yule mwanamke akamwambia, “Bwana, tafadhali nipe maji hayo ili nisipate kiu tena na wala nisije tena hapa kuteka maji!”
16Isa akamjibu, “Nenda ukamwite mumeo, uje naye hapa.”
17Yule mwanamke akajibu, “Sina mume.”
Isa akamwambia, “Umesema kweli kuwa huna mume. 18Kwa maana umeshakuwa na wanaume watano na mwanaume unayeishi naye sasa si mume wako! Umesema ukweli.”
19 Yule mwanamke akasema, “Bwana, naona bila shaka wewe ni nabii. 20 Baba zetu waliabudu kwenye mlima huu, lakini ninyi Wayahudi mnasema ni lazima tukaabudu huko Yerusalemu.”
21 Isa akamjibu, “Mwanamke, niamini, wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba#4:21 Jina Baba linaonyesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. katika mlima huu, wala huko Yerusalemu. 22 Ninyi Wasamaria mnaabudu msichokijua. Sisi Wayahudi tunamwabudu Mungu tunayemjua kwa sababu wokovu unatoka kwa Wayahudi. 23 Lakini saa yaja, tena ipo, ambapo wale waabuduo halisi, watamwabudu Baba katika roho na kweli. Watu wanaoabudu namna hii, ndio Baba anawatafuta. 24 Mungu ni Roho na wote wanaomwabudu imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.”
25 Yule mwanamke akamwambia, “Ninafahamu kwamba Masiya (aitwaye Al-Masihi) anakuja. Yeye akija, atatueleza mambo yote.”
26 Isa akamwambia, “Mimi ninayezungumza nawe, ndiye.”
27 Wakati huo wanafunzi wake wakarudi, wakashangaa sana kumwona akizungumza na mwanamke. Lakini hakuna aliyemuuliza, “Unataka nini kwake?” Au “Kwa nini unazungumza naye?”
28Yule mwanamke akaacha mtungi wake, akarudi mjini akawaambia watu, 29 “Njooni mkamwone mtu aliyeniambia kila kitu nilichotenda! Je, yawezekana huyu ndiye Al-Masihi?” 30Basi wakamiminika watu kutoka mjini wakamwendea Isa.
31 Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wakimsihi, “Mwalimu, kula angalau chochote.”
32 Lakini yeye akawajibu, “Mimi ninacho chakula ambacho ninyi hamkifahamu.”
33Basi wanafunzi wakaanza kuulizana, “Kuna mtu ambaye amemletea chakula?” 34 Lakini Isa akawajibu, “Chakula changu ni kufanya mapenzi ya Mungu ambaye amenituma na kuikamilisha kazi yake. 35 Je, ninyi hamsemi, ‘Bado miezi minne tuvune?’ Inueni macho yenu myaangalie mashamba jinsi mazao yalivyo tayari kuvunwa! 36 Mvunaji tayari anapokea mshahara wake, naye anakusanya mazao kwa ajili ya uzima wa milele. Ili yeye apandaye na yeye avunaye wafurahi pamoja. 37 Hivyo kule kusema, ‘Mmoja hupanda na mwingine huvuna,’ ni kweli kabisa. 38Niliwatuma mkavune mazao ambayo hamkupanda, wengine walifanya kazi ngumu, nanyi mmevuna faida ya taabu yao.”
Wasamaria Wengi Waamini
39 Wasamaria wengi katika mji ule wakamwamini Isa kwa sababu ya ushuhuda wa yule mwanamke alipowaambia kwamba, “Ameniambia kila kitu nilichotenda.” 40Hivyo wale Wasamaria walipomjia, wakamsihi akae kwao. Naye akakaa huko siku mbili. 41Kwa sababu ya neno lake, watu wengi wakaamini.
42 Wakamwambia yule mwanamke, “Sasa tunaamini, wala si kwa sababu ya maneno yako tu, bali kwa kuwa tumemsikia sisi wenyewe. Tumejua hakika kweli ya kwamba huyu ndiye Al-Masihi, Mwokozi wa ulimwengu.”
Isa Amponya Mwana Wa Afisa
43Baada ya zile siku mbili, Isa aliondoka kwenda Galilaya. 44 (Basi Isa mwenyewe alikuwa amesema kwamba nabii hapati heshima katika nchi yake mwenyewe.) 45 Alipofika Galilaya, Wagalilaya walimkaribisha, kwani walikuwa wameona yale aliyoyatenda huko Yerusalemu wakati wa Sikukuu ya Pasaka. Kwa maana wao pia walikuwa wamehudhuria hiyo Sikukuu.
46 Hivyo Isa akaja tena mpaka Kana ya Galilaya, kule alikokuwa amebadili maji kuwa divai. Huko kulikuwepo na afisa mmoja wa mfalme, ambaye mwanawe alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. 47 Huyo mtu aliposikia kwamba Isa alikuwa amewasili Galilaya kutoka Uyahudi, alimwendea na kumwomba ili aje kumponya mwanawe, aliyekuwa mgonjwa karibu ya kufa.
48 Isa akamwambia, “Ninyi watu msipoona ishara na miujiza kamwe hamtaamini.”
49Yule afisa wa mfalme akamwambia, “Bwana, tafadhali shuka kabla mwanangu hajafa.”
50Isa akamjibu, “Enenda zako, mwanao yu hai.”
Yule afisa akaamini yale maneno Isa aliyomwambia, akaondoka akaenda zake. 51Alipokuwa bado yuko njiani, akakutana na watumishi wake wakamwambia kwamba mwanawe yu mzima. 52Akawauliza saa ambayo alianza kupata nafuu. Wakamwambia, “Jana yapata saa saba, homa ilimwacha.”
53 Ndipo baba wa huyo mtoto akakumbuka kuwa huo ndio wakati ambapo Isa alikuwa amemwambia, “Mwanao yu hai.” Kwa hiyo yeye, pamoja na wote wa nyumbani mwake wakamwamini Isa.
54 Hii ilikuwa ishara ya pili ambayo Isa alifanya aliporudi Galilaya kutoka Uyahudi.

Àwon tá yàn lọ́wọ́lọ́wọ́ báyìí:

Yohana 4: NMM

Ìsàmì-sí

Pín

Daako

None

Ṣé o fẹ́ fi àwọn ohun pàtàkì pamọ́ sórí gbogbo àwọn ẹ̀rọ rẹ? Wọlé pẹ̀lú àkántì tuntun tàbí wọlé pẹ̀lú àkántì tí tẹ́lẹ̀

Àwọn fídíò fún Yohana 4