Mattayo MT. 17
17
1NA baada ya siku sita Yesu akawachukua Petro, na Yakobo, na Yohana ndugu yake, akawaleta juu ya mlima mrefu peke yao; 2akageuka sura yake mbele yao: uso wake ukangʼaa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. 3Wakawatokea Musa na Eliya, wakizumgumza nae. 4Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka tutafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya. 5Alipokuwa akisema, wingu jeupe likawatia uvuli; sauti ikatoka katika lile wingu, ikinena, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, niliyependezwa nae; msikieni yeye. 6Na wale wanafunzi waliposikia, wakaanguka kifudifudi, wakaogopa sana. 7Yesu akaja, akawagusa, akasema, Ondokeni, msiogope. 8Wakainua macho yao, wasione mtu illa Yesu peke yake.
9Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu akawaagiza, akinena, Msimwambie mtu khabari ya mambo hayo, hatta Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu. 10Wanafunzi wake wakamwuliza, wakinena, Mbona bassi waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? 11Yesu akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, nae atatengeneza yote; 12lakini nawaambieni, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu nae atateswa nao. 13Ndipo wakafahamu wale wanafunzi ya kuwa amesema nao khabari za Yohana Mbatizaji.
14Nao walipoufikia mkutano, mtu akamjia, akampigia magoti, akinena, 15Bwana, mrehemu mwana wangu, kwa kuwa hushikwa na kifafa, na kuteswa vibaya: maana marra nyingi huanguka motoni, na marra nyingi majini. 16Nikamleta kwa wanafunzi wako, nao hawakuweza kumponya. 17Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini na kipotofu, nitakuwa pamoja nanyi hatta lini? Nitachukuliana nanyi hatta lini? Mleteni huku kwangu. 18Yesu akamkaripia pepo, akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. 19Kiisha wale wanafunzi wakaniwendea Yesu kwa feragha, wakasema, Mbona sisi hatukuweza kumfukuza? 20Yesu akawaambia, Kwa sababu ya kutokuamini kwenu. Kwa maana, amin, nawaambieni, Mkiwa na imani kama punje ya kharadali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa hatta kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. 21Lakini namna hii haitoki illa kwa kusali na kufunga.
22Walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu karibu atatiwa mikononi mwa watu, 23nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana.
24Hatta walipofika Kapernaum, wale watozao nussu shekeli wakamwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nussu shekeli? 25Akanena, Hutoa. Nae alipoingia nyumbani, Yesu akatangulia kumwuliza, akinena, Waonaje, Simon? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? kwa wana wao au kwa wageni? 26Petro akamwambia, Kwa wageni. Yesu akamwambia, Bassi, kama ni hivyo, wana ni huru. 27Lakini tusije tukawachukiza, enenda baharini ukatumbukize ndoana, ukatwae samaki yule azukae kwanza; na ukifunua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako.
Àwon tá yàn lọ́wọ́lọ́wọ́ báyìí:
Mattayo MT. 17: SWZZB1921
Ìsàmì-sí
Pín
Daako
Ṣé o fẹ́ fi àwọn ohun pàtàkì pamọ́ sórí gbogbo àwọn ẹ̀rọ rẹ? Wọlé pẹ̀lú àkántì tuntun tàbí wọlé pẹ̀lú àkántì tí tẹ́lẹ̀
Swahili New Testament © Bible Society of Tanzania, 1921.