YouVersion Logo
تلاش

Mwanzo 18

18
Wageni Watatu
1 bwana akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre wakati alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri. 2 Ibrahimu akainua macho akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, aliharakisha kutoka kwenye ingilio la hema lake kuwalaki na kuwasujudia hadi nchi.
3Akasema, “Kama nimepata kibali machoni penu, ee bwana wangu, usimpite mtumishi wako. 4 Acha yaletwe maji kidogo, kisha ninyi nyote mnawe miguu yenu na mpumzike chini ya mti huu. 5 Niruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.”
Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.”
6 Hivyo Ibrahimu akaharakisha akaingia hemani kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”
7 Kisha Ibrahimu akakimbia kwenda kwenye kundi, akachagua ndama mzuri, laini na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha. 8 Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.
9 Wakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?”
Akasema, “Yuko huko, ndani ya hema.”
10 Kisha bwana akasema, “Hakika nitakurudia tena majira kama haya mwakani na Sara mkeo atakuwa ana mwana.”
Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema, lililokuwa nyuma yake. 11 Ibrahimu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. 12 Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”
13 Ndipo bwana akamwambia Ibrahimu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ 14 Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa bwana? Nitakurudia mwakani majira kama haya, naye Sara atakuwa na mwana.”
15Sara akaogopa kwa kuwa alidanganya na kusema, “Mimi sikucheka.”
Lakini Bwana akasema, “Ndiyo, ulicheka!”
Ibrahimu Aiombea Sodoma
16Wakati watu hao waliposimama ili waondoke, walielekeza nyuso zao Sodoma, Ibrahimu akawatoa kitambo kidogo ili awasindikize. 17 Ndipo bwana akasema, “Je, nimfiche Ibrahimu jambo ninalokusudia kufanya? 18 Hakika Ibrahimu atakuwa taifa kubwa na lenye nguvu, kupitia kwake mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. 19 Kwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya bwana, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili bwana atimize ahadi yake kwa Ibrahimu.”
20 Basi bwana akasema, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi yao inasikitisha sana, 21 kwamba nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.”
22 Basi wale watu wakageuka wakaenda kuelekea Sodoma, lakini Ibrahimu akabaki amesimama mbele za bwana. 23 Ndipo Ibrahimu akamsogelea akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? 24 Je, ikiwa watakuwepo watu wenye haki hamsini katika mji huo, hivi kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo ndani yake? 25 Hilo na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo, kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Iwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya lililo sawa?”
26 bwana akasema, “Kama nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitausamehe huo mji wote kwa ajili yao.”
27 Kisha Ibrahimu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu; 28je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?”
Bwana akamwambia, “Kama nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.”
29Ibrahimu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?”
Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.”
30 Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?”
Akajibu, “Sitapaangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.”
31Ibrahimu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, kama wakipatikana huko watu ishirini tu?”
Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”
32 Ibrahimu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?”
Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.”
33 bwana alipomaliza kuzungumza na Ibrahimu, akaondoka, naye Ibrahimu akarudi nyumbani kwake.

موجودہ انتخاب:

Mwanzo 18: NMM

سرخی

شئیر

کاپی

None

کیا آپ جاہتے ہیں کہ آپ کی سرکیاں آپ کی devices پر محفوظ ہوں؟ Sign up or sign in