Injili Ulimwenguni - Sehemu 1Mfano
Matthew 1:18-25
Basi Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi: Maria mama yake alikuwa ameposwa na Yosefu, lakini kabla hawajakutana kimwili, Maria alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu.Kwa kuwa Yosefu, mwanaume aliyekuwa amemposa alikuwa mtu mwadilifu, hakutaka kumwaibisha Maria hadharani, aliazimu kumwacha kwa siri.
Lakini mara alipoazimu kufanya jambo hili, malaika wa Bwana akamtokea katika ndoto na kusema,
“Yosefu mwana wa Daudi, usiogope kumchukua Maria awe mke wako, kwa maana mimba aliyo nayo ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu.Naye atamzaa mwana, nawe utamwita Jina lake Yesu, kwa maana yeye ndiye atakayewaokoa watu wake kutoka katika dhambi zao.”
Haya yote yametukia ili litimie lile Bwana alilokuwa amenena kupitia nabii, akisema:
“Tazama, bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, nao watamwita Jina lake Imanueli,” maana yake, “Mungu pamoja nasi.”
Yosefu alipoamka kutoka usingizini, akafanya kama vile alivyoagizwa na malaika wa Bwana, akamchukua Maria kuwa mke wake.
Lakini hawakukutana kimwili mpaka Maria alipojifungua mwanawe kifungua mimba akamwita Jina lake Yesu.
Luke 2:1-20
Siku zile Kaisari Augusto alitoa amri kwamba watu wote waandikishwe katika ulimwengu wa Kirumi.Orodha hii ndiyo ya kwanza iliyofanyika wakati Krenio alipokuwa mtawala wa Shamu Kila mtu alikwenda kuandikishwa katika mji wake alikozaliwa.
Hivyo Yosefu akapanda kutoka mji wa Nazareti ulioko Galilaya kwenda Uyahudi, mpaka Bethlehemu, mji wa Daudi, kwa sababu yeye alikuwa wa ukoo na wa nyumba ya Daudi.
Alikwenda huko kujiandikisha pamoja na Maria, ambaye alikuwa amemposa naye alikuwa mjamzito.
Wakiwa Bethlehemu, wakati wa Maria wa kujifungua ukawa umetimia. Naye akamzaa mwanawe, kifungua mimba. Akamfunika nguo za kitoto na kumlaza katika hori ya kulia ng'ombe, kwa sababu hapakuwa na nafasi katika nyumba ya wageni.
Katika eneo lile walikuwako wachungaji waliokuwa wakikaa mashambani, wakilinda makundi yao ya kondoo usiku.Ghafula tazama, malaika wa Bwana akawatokea, nao utukufu wa Bwana ukawang'aria kotekote, wakaingiwa na hofu. Lakini malaika akawaambia, “Msiogope. Kwa maana tazama nawaletea habari njema za furaha itakayokuwa kwa watu wote.Leo katika mji wa Daudi kwa ajili yenu amezaliwa Mwokozi, ndiye Kristo Bwana.Hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu: Mtamkuta mtoto mchanga amefunikwa nguo za kitoto na kulazwa katika hori ya kulia ng'ombe.”Ghafula pakawa na jeshi kubwa la mbinguni pamoja na huyo malaika wakimsifu Mungu wakisema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.” Hao malaika walipokwisha kuondoka na kwenda zao mbinguni, wale wachungaji wakasemezana wao kwa wao wakisema, “Twendeni Bethlehemu tukaone mambo haya ya ajabu yaliyotukia, ambayo Bwana ametuambia habari zake.” Hivyo wakaenda haraka Bethlehemu, wakawakuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga akiwa amelala katika hori la kulia ng'ombe.Walipomwona yule mtoto, wakawaeleza yale waliyokuwa wameambiwa kuhusu huyu mtoto. Nao wote waliosikia habari hizi wakastaajabia yale waliyoambiwa na wale wachungaji wa kondoo. Lakini Maria akayaweka mambo haya yote moyoni mwake na kuyatafakari. Wale wachungaji wakarudi, huku wakimtukuza Mungu na kumsifu kwa ajili ya mambo yote waliyokuwa wameambiwa na kuyaona.
Matthew 2:1-23
Baada ya Yesu kuzaliwa katika mji wa Bethlehemu huko Uyahudi, wakati wa utawala wa Mfalme Herode,
wataalamu wa mambo ya nyota kutoka mashariki walifika Yerusalemu wakiuliza, “Yuko wapi huyo aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tumeona nyota yake ikitokea mashariki, nasi tumekuja kumwabudu.” Mfalme Herode aliposikia jambo hili aliingiwa na hofu sana pamoja na watu wote wa Yerusalemu. Herode akawaita pamoja makuhani wakuu na walimu wa sheria, akawauliza ni mahali gani ambapo Kristo angezaliwa. Nao wakamwambia, “Katika Uyahudi, kwa maana hivyo ndivyo ilivyoandikwa na nabii:“ ‘Nawe, Bethlehemu, katika nchi ya Yuda,wewe si mdogo miongoni mwa watawala wa Yuda,kwa maana kutoka kwako atakuja mtawala atakayekuwa mchungaji wa watu wangu Israeli.’ ”
"Ndipo Herode akawaita wale wataalamu wa nyota kwa siri na kutaka kujua kutoka kwao uhakika kamili wa wakati ile nyota ilipoonekana.Kisha akawatuma waende Bethlehemu akiwaambia,
“Nendeni mkamtafute kwa bidii huyo mtoto. Nanyi mara mumwonapo, mniletee habari ili na mimi niweze kwenda kumwabudu.” Baada ya kumsikia mfalme, wale wataalamu wa nyota wakaenda zao, nayo ile nyota waliyoiona mashariki ikawatangulia, nao wakaifuata mpaka iliposimama mahali pale alipokuwa mtoto.Walipoiona ile nyota wakajawa na furaha kubwa mno. Walipoingia ndani ya ile nyumba, wakamwona mtoto pamoja na Maria mama yake, wakamsujudu na kumwabudu yule mtoto Yesu. Ndipo wakafungua hazina zao, wakamtolea zawadi za dhahabu, uvumba na manemane.
Nao wakiisha kuonywa katika ndoto wasirudi kwa Herode, wakarudi kwenda katika nchi yao kwa njia nyingine. Walipokwisha kwenda zao, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto akamwambia,
“Ondoka, mchukue mtoto na mama yake mkimbilie Misri. Kaeni huko mpaka nitakapowaambia, kwa maana Herode anataka kumtafuta huyu mtoto ili amuue.”Kisha Yosefu akaondoka, akamchukua mtoto pamoja na mama yake wakati wa usiku, nao wakaenda Misri ambako walikaa mpaka Herode alipokufa. Hili lilikuwa, ili litimie lile lililonenwa na Bwana kwa kinywa cha nabii kusema, “Kutoka Misri nilimwita mwanangu.”
Herode alipong'amua kwamba wale wataalamu wa nyota wamemshinda kwa akili, alikasirika sana, naye akatoa amri ya kuwaua watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili kurudi chini katika mji wa Bethlehemu na sehemu zote za jirani, kufuatana na ule muda alioambiwa na wale wataalamu wa nyota.
Ndipo lilipotimia neno lililonenwa na nabii Yeremia.“Sauti ilisikika huko Rama,kilio cha huzuni na maombolezo makuu,Raheli akilia kwa ajili ya wanawe,akikataa kufarijiwa, kwa sababu hawako tena.” Baada ya Herode kufa, malaika wa Bwana akamtokea Yosefu katika ndoto huko Misri na kusema, “Ondoka, mchukue mtoto na mama mwende, mrudi katika nchi ya Israeli kwa sababu wale waliokuwa wanatafuta uhai wa mtoto wamekufa.”
Basi Yosefu, akaondoka akamchukua mtoto na mama yake wakaenda mpaka nchi ya Israeli.Lakini aliposikia kwamba Arkelao alikuwa anatawala huko Uyahudi mahali pa Herode baba yake, aliogopa kwenda huko. ANaye akiisha kuonywa katika ndoto, akaenda zake sehemu za Galilaya.
Kuhusu Mpango huu
Mfuatano huu ni kusanyiko la hadithi kuhusu maisha Kristo itakayoshirikisha watazamaji wote ulimwenguni kwa kutumia mchanganyiko wa kuona na sauti. Maisha na mafundisho ya Yesu yalidhihirishwa katika kitabu hiki cha hadithi ambacho kinafuata masimulizi ya Agano Jipya yanayopatikana katika vitabu vya Injili vya Mathayo, Marko, Luka, na Yohana.
More
Tungependa kumshukuru GNPI Afrika kwa kutoa mpango huu. Kwa habari zaidi, tafadhali tembelea:
http://gnpi-africa.org/