Zekaria 11:4-17
Zekaria 11:4-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alisema hivi: “Jifanye mchungaji wa kondoo waendao kuchinjwa. Wanunuzi wao wanawachinja lakini hawaadhibiwi; na wauzaji wao wanasema, ‘Na ashukuriwe Mwenyezi-Mungu! Sasa tumetajirika’. Hata wachungaji wenyewe hawawaonei huruma. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba, sitawahurumia tena wakazi wa dunia. Nitamwacha kila mtu mikononi mwa mwenzake, na kila raia mikononi mwa mfalme wake. Nao wataiangamiza dunia, nami sitamwokoa yeyote mikononi mwao.” Basi, nikawa mchungaji wa kondoo waliokuwa wanakwenda kuchinjwa, kwani niliajiriwa na wale waliofanya biashara ya kondoo. Nikachukua fimbo mbili: Moja nikaiita “Fadhili,” na nyingine nikaiita “Umoja,” nikaenda kuchunga kondoo. Kwa muda wa mwezi mmoja, nikaua wachungaji watatu wabaya. Tena uvumilivu wangu kwa kondoo ukaniishia, nao kwa upande wao, wakanichukia. Basi, nikawaambia, “Sitakuwa mchungaji wenu tena. Atakayekufa na afe! Atakayeangamia na aangamie! Na wale watakaobaki na watafunane wao kwa wao.” Nikaichukua ile fimbo yangu niliyoiita “Fadhili,” nikaivunja, kuonesha kwamba agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na watu wake limevunjwa. Na agano hilo likavunjwa siku hiyohiyo. Wale wafanyabiashara ya kondoo waliokuwa wananiangalia, wakajua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa ameongea kwa matendo yangu. Kisha nikawaambia, “Kama mnaona kuwa ni sawa, nilipeni ujira wangu; lakini kama mnaona sivyo, basi kaeni nao.” Basi, wakanipimia vipande thelathini vya fedha mshahara wangu. Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Ziweke katika hazina ya hekalu.” Mshahara huo ulikuwa ni malipo halali kwa kazi yangu. Hivyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha, nikazitia katika hazina ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. Kisha nikaivunja ile fimbo yangu ya pili niliyoiita “Umoja;” na hivyo nikauvunja umoja kati ya Yuda na Israeli. Mwenyezi-Mungu akaniambia tena, “Jifanye tena mchungaji, lakini safari hii uwe kama mchungaji mbaya! Maana nitaleta nchini mchungaji asiyemjali kondoo anayeangamia, au kumtafuta kondoo anayetangatanga, au kumtibu aliyejeruhiwa wala kumlisha aliye hai: Bali atakula wale kondoo wanono, hata kwato zao. “Ole wake mchungaji mbaya, ambaye anawaacha kondoo wake! Upanga na uukate mkono wake, na jicho lake la kulia na ling'olewe! Mkono wake na udhoofike, jicho lake la kulia na lipofuke.”
Zekaria 11:4-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
BWANA, Mungu wangu, alisema hivi, Lilishe kundi la machinjo, ambalo wenye kundi hilo huwachinja, kisha hujiona kuwa hawana hatia; na hao wawauzao husema, Na ahimidiwe BWANA, kwa maana mimi ni tajiri; na wachungaji wao wenyewe hawawahurumii. Maana mimi sitawahurumia tena wenyeji wa nchi hii, asema BWANA; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao, mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala mimi sitawaokoa mikononi mwao. Basi nikalilisha kundi la machinjo, kweli kondoo waliokuwa wanyonge kabisa. Kisha nikajipatia fimbo mbili; nami nikaiita ya kwanza, Neema, na ya pili nikaiita, Vifungo; nikalilisha kundi lile. Nami nikawakatilia mbali wachungaji watatu katika mwezi mmoja; maana nafsi yangu ilikuwa imechoka kwa ajili yao, na nafsi zao pia walinichukia. Ndipo nikasema, Sitawalisheni; afaye na afe; atakayekatiliwa mbali na akatiliwe mbali; nao waliosalia, kila mmoja na ale nyama ya mwili wa mwenziwe. Nikaitwaa hiyo fimbo yangu, iitwayo Neema, nikaikata vipande viwili, ili nipate kulivunja agano langu nililolifanya na watu wa kabila zote. Nayo ikavunjwa siku ile; na hivyo wale kondoo wanyonge walionisikiliza wakajua ya kuwa neno hili ndilo neno la BWANA. Nikawaambia, Mkiona vema, nipeni ujira wangu; kama sivyo, msinipe. Basi wakanipimia vipande thelathini vya fedha, kuwa ndio ujira wangu. Kisha BWANA akaniambia, Mtupie mfinyanzi kima kizuri, hicho nilichotiwa kima na watu hao. Basi nikavitwaa vile vipande thelathini vya fedha, nikamtupia huyo mfinyanzi ndani ya nyumba ya BWANA. Ndipo nikaikata vipande viwili fimbo yangu ya pili, iitwayo Vifungo, ili nipate kuuvunja udugu uliokuwa kati ya Yuda na Israeli. BWANA akaniambia, Jitwalie tena vyombo vya mchungaji mpumbavu. Kwa maana, tazama, mimi nitainua katika nchi hii mchungaji, ambaye hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuzirarua-rarua kwato zao. Ole wake mchungaji asiyefaa, aliachaye kundi! Upanga utakuwa juu ya mkono wake, na juu ya jicho lake la kuume; mkono wake utakuwa umekauka kabisa, na jicho lake la kuume litakuwa limepofuka.
Zekaria 11:4-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
BWANA, Mungu wangu, alisema hivi, Lilishe kundi la machinjo, ambalo wenye kundi hilo huwachinja, kisha hujiona kuwa hawana hatia; na hao wawauzao husema, Na ahimidiwe BWANA, kwa maana mimi ni tajiri; na wachungaji wao wenyewe hawawahurumii. Maana mimi sitawahurumia tena wenyeji wa nchi hii, asema BWANA; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao, mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala mimi sitamwokoa yeyote kutoka kwa mkono wao. Basi nikalilisha kundi la machinjo, kweli kondoo waliokuwa wanyonge kabisa. Kisha nikajipatia fimbo mbili; nami nikaiita ya kwanza, Neema, na ya pili nikaiita, Umoja; nikalilisha kundi lile. Nami nikawakatilia mbali wachungaji watatu katika mwezi mmoja; maana nafsi yangu ilikuwa imechoka kwa ajili yao, na nafsi zao pia walinichukia. Ndipo nikasema, Sitawalisheni; afaye na afe; atakayekatiliwa mbali na akatiliwe mbali; nao waliosalia, kila mmoja na ale nyama ya mwili wa mwenziwe. Nikaitwaa hiyo fimbo yangu, iitwayo Neema, nikaikata vipande viwili, ili nipate kulivunja agano langu nililolifanya na watu wa kabila zote. Nayo ikavunjwa siku ile; na hivyo wale kondoo wanyonge walionisikiliza wakajua ya kuwa neno hili ndilo neno la BWANA. Nikawaambia, Mkiona vema, nipeni ujira wangu; kama sivyo, msinipe. Basi wakanipimia vipande thelathini vya fedha, kuwa ndio ujira wangu. Kisha BWANA akaniambia, Mtupie mfinyanzi kima kizuri, hicho nilichotiwa kima na watu hao. Basi nikavitwaa vile vipande thelathini vya fedha, nikamtupia huyo mfinyanzi ndani ya nyumba ya BWANA. Ndipo nikaikata vipande viwili fimbo yangu ya pili, iitwayo Umoja, ili nipate kuuvunja udugu uliokuwa kati ya Yuda na Israeli. BWANA akaniambia, Jitwalie tena vyombo vya mchungaji mpumbavu. Kwa maana, tazama, mimi nitainua katika nchi hii mchungaji, ambaye hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuziraruararua kwato zao. Ole wake mchungaji asiyefaa, aliachaye kundi! Upanga utakuwa juu ya mkono wake, na juu ya jicho lake la kulia; mkono wake utakuwa umekauka kabisa, na jicho lake la kulia litakuwa limepofuka.
Zekaria 11:4-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hili ndilo asemalo BWANA Mungu wangu: “Lilishe kundi lililokusudiwa kuchinjwa. Wanunuzi wake huwachinja na kuondoka pasipo kuadhibiwa. Wale wanaowauza husema, ‘BWANA asifiwe, mimi ni tajiri!’ Wachungaji wao wenyewe hawawahurumii. Kwa kuwa sitawahurumia tena watu wa nchi,” asema BWANA. “Nitawakabidhi kila mtu mkononi mwa jirani yake na mfalme wake. Wataitenda jeuri nchi, nami sitawaokoa kutoka mikononi mwao.” Kwa hiyo nikalilisha kundi lililotiwa alama kwa kuchinjwa, hasa kundi lililoonewa sana. Kisha nikachukua fimbo mbili, moja nikaiita Fadhili na nyingine Umoja, nami nikalilisha kundi. Katika mwezi mmoja nikawaondoa wachungaji watatu. Kundi la kondoo likanichukia, nami nikachoshwa nao, nikasema, “Sitakuwa mchungaji wenu. Waache wanaokufa wafe na wanaoangamia waangamie. Wale waliobakia kila mmoja na ale nyama ya mwenzake.” Kisha nikachukua fimbo yangu inayoitwa Fadhili nikaivunja, kutangua Agano nililofanya na mataifa yote. Likatanguka siku hiyo, kwa hiyo wale waliodhurika katika kundi, waliokuwa wakiniangalia wakajua kuwa hilo lilikuwa neno la BWANA. Nikawaambia, “Mkiona kuwa ni vyema, nipeni ujira wangu, la sivyo, basi msinipe.” Kwa hiyo wakanilipa vipande thelathini vya fedha. Naye BWANA akaniambia, “Mtupie mfinyanzi,” hiyo bei nzuri waliyonithaminia! Kwa hiyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha na kumtupia huyo mfinyanzi katika nyumba ya BWANA. Kisha nikaivunja fimbo yangu ya pili iitwayo Umoja, kuvunja undugu kati ya Yuda na Israeli! Kisha BWANA akaniambia, “Vitwae tena vifaa vya mchungaji mpumbavu. Kwa maana ninakwenda kumwinua mchungaji juu ya nchi ambaye hatamjali aliyepotea, wala kuwatafuta wale wachanga au kuwaponya waliojeruhiwa, wala kuwalisha wenye afya, lakini atakula nyama ya kondoo wanono na kuzirarua kwato zao. “Ole wa mchungaji asiyefaa, anayeliacha kundi! Upanga na uupige mkono wake na jicho lake la kuume! Mkono wake na unyauke kabisa, jicho lake la kuume lipofuke kabisa!”