Zekaria 11:4-17
Zekaria 11:4-17 BHN
Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu, alisema hivi: “Jifanye mchungaji wa kondoo waendao kuchinjwa. Wanunuzi wao wanawachinja lakini hawaadhibiwi; na wauzaji wao wanasema, ‘Na ashukuriwe Mwenyezi-Mungu! Sasa tumetajirika’. Hata wachungaji wenyewe hawawaonei huruma. Mimi Mwenyezi-Mungu nasema kwamba, sitawahurumia tena wakazi wa dunia. Nitamwacha kila mtu mikononi mwa mwenzake, na kila raia mikononi mwa mfalme wake. Nao wataiangamiza dunia, nami sitamwokoa yeyote mikononi mwao.” Basi, nikawa mchungaji wa kondoo waliokuwa wanakwenda kuchinjwa, kwani niliajiriwa na wale waliofanya biashara ya kondoo. Nikachukua fimbo mbili: Moja nikaiita “Fadhili,” na nyingine nikaiita “Umoja,” nikaenda kuchunga kondoo. Kwa muda wa mwezi mmoja, nikaua wachungaji watatu wabaya. Tena uvumilivu wangu kwa kondoo ukaniishia, nao kwa upande wao, wakanichukia. Basi, nikawaambia, “Sitakuwa mchungaji wenu tena. Atakayekufa na afe! Atakayeangamia na aangamie! Na wale watakaobaki na watafunane wao kwa wao.” Nikaichukua ile fimbo yangu niliyoiita “Fadhili,” nikaivunja, kuonesha kwamba agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na watu wake limevunjwa. Na agano hilo likavunjwa siku hiyohiyo. Wale wafanyabiashara ya kondoo waliokuwa wananiangalia, wakajua kwamba Mwenyezi-Mungu alikuwa ameongea kwa matendo yangu. Kisha nikawaambia, “Kama mnaona kuwa ni sawa, nilipeni ujira wangu; lakini kama mnaona sivyo, basi kaeni nao.” Basi, wakanipimia vipande thelathini vya fedha mshahara wangu. Kisha Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Ziweke katika hazina ya hekalu.” Mshahara huo ulikuwa ni malipo halali kwa kazi yangu. Hivyo nikachukua hivyo vipande thelathini vya fedha, nikazitia katika hazina ya hekalu la Mwenyezi-Mungu. Kisha nikaivunja ile fimbo yangu ya pili niliyoiita “Umoja;” na hivyo nikauvunja umoja kati ya Yuda na Israeli. Mwenyezi-Mungu akaniambia tena, “Jifanye tena mchungaji, lakini safari hii uwe kama mchungaji mbaya! Maana nitaleta nchini mchungaji asiyemjali kondoo anayeangamia, au kumtafuta kondoo anayetangatanga, au kumtibu aliyejeruhiwa wala kumlisha aliye hai: Bali atakula wale kondoo wanono, hata kwato zao. “Ole wake mchungaji mbaya, ambaye anawaacha kondoo wake! Upanga na uukate mkono wake, na jicho lake la kulia na ling'olewe! Mkono wake na udhoofike, jicho lake la kulia na lipofuke.”