Zekaria 1:1-21
Zekaria 1:1-21 Biblia Habari Njema (BHN)
Mnamo mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa mfalme Dario wa Persia, neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido: “Mimi Mwenyezi-Mungu nilichukizwa sana na wazee wenu. Basi, waambie watu kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nasema hivi: Nirudieni, nami nitawarudieni nyinyi. Msiwe kama wazee wenu ambao manabii waliwaambia waachane na mienendo yao miovu na matendo yao mabaya, lakini wao hawakunisikiliza wala hawakunitii mimi Mwenyezi-Mungu. Wazee wenu, wako wapi? Na manabii, je, wanaishi milele? Je, wazee wenu hawakupata adhabu kwa sababu ya kukataa maagizo yangu na amri nilizowapa kwa njia ya watumishi wangu manabii? Wakati huo, wao walitubu na kusema kuwa mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, nilikusudia kuwatenda kulingana na mienendo yao na matendo yao, na kweli ndivyo nilivyowatenda.” Mnamo siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi wa Shebati, mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia mimi nabii Zekaria mwana wa Berekia, mjukuu wa Ido, kama ifuatavyo: Wakati wa usiku, nilimwona malaika amepanda farasi mwekundu. Malaika huyo alikuwa amesimama bondeni, katikati ya miti ya mihadasi. Nyuma yake kulikuwa na farasi wengine wekundu, wa kijivujivu na weupe. Basi, nikamwuliza, “Bwana, Farasi hawa wanamaanisha nini?” Malaika huyo aliyeongea nami akaniambia, “Nitakuonesha hao farasi wanamaanisha nini. Hawa ndio waliotumwa na Mwenyezi-Mungu kuikagua dunia.” Hao farasi wakamwambia huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumeikagua dunia yote, nayo kweli imetulia.” Ndipo huyo malaika wa Mwenyezi-Mungu akasema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kwa muda gani utaendelea kutokuwa na huruma juu ya mji wa Yerusalemu na miji ya nchi ya Yuda ambayo umeikasirikia kwa muda wa miaka sabini?” Mwenyezi-Mungu akampa huyo malaika jibu jema na lenye matumaini. Basi, huyo malaika akaniambia, “Unapaswa kutangaza kwa sauti kwamba Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Moyo wangu umejaa upendo kwa mji wa Yerusalemu, naam, kwa mlima Siyoni. Walakini nimechukizwa sana na mataifa ambayo yanastarehe. Kweli niliwakasirikia Waisraeli kidogo, lakini mataifa hayo yaliwaongezea maafa. Kwa hiyo, nasema mimi Mwenyezi-Mungu, naurudia mji wa Yerusalemu kwa huruma; humo itajengwa nyumba yangu, na ujenzi mpya wa mji utaanza.’” Kisha malaika huyo akaniambia nitangaze ujumbe huu mwingine: “Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: ‘Miji yangu itafurika tena fanaka. Mimi Mwenyezi-Mungu nitaufariji tena mji wa Siyoni; nitauteua mji wa Yerusalemu kuwa wangu.’” Katika maono mengine, niliona pembe nne. Nami nikamwuliza yule malaika aliyezungumza nami, “Pembe hizi zinamaanisha nini?” Yeye akanijibu, “Pembe hizi zinamaanisha yale mataifa ambayo yaliwatawanya watu wa Yuda, Israeli na Yerusalemu.” Kisha, Mwenyezi-Mungu akanionesha wafuachuma wanne. Nami nikauliza, “Watu hawa wanakuja kufanya nini?” Yeye akanijibu, “Watu hawa wamekuja kuyatisha na kuyaangamiza yale mataifa yenye nguvu ambayo yaliishambulia nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”
Zekaria 1:1-21 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Katika mwezi wa nane, mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, BWANA amewakasirikia sana baba zenu. Basi, uwaambie, BWANA wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema BWANA wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunitii, asema BWANA. Je, Baba zenu wako wapi? Je, manabii nao wanaishi milele? Lakini maneno yangu, na amri zangu nilizowaagiza hao manabii, watumishi wangu, je, Hazikuwapata baba zenu? Nao wakatubu na kusema, BWANA wa majeshi ametutenda kulingana na njia zetu, na matendo yetu, kama alivyokusudia kutenda. Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, Niliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya miti ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe. Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonesha ni nini hawa. Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio BWANA aliowatuma, waende huku na huko duniani. Nao wakamjibu yule malaika wa BWANA aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huku na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe. Ndipo yule malaika wa BWANA akajibu, akasema, Ee BWANA wa majeshi, hadi lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini? Naye BWANA akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja. Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana. Nami ninayakasirikia sana mataifa yanayostarehe; kwa maana mimi nilikuwa nimekasirika kidogo tu, nao wakayazidisha maafa. Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema BWANA wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu. Piga kelele tena, na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Miji yangu itajawa na ufanisi tena; naye BWANA ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena. Nami nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, pembe nne. Nami nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Nini hizi? Naye akanijibu, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, na Israeli, na Yerusalemu. Kisha BWANA akanionesha wafua chuma wanne. Ndipo nikauliza, Hawa wanakuja kufanya nini? Akasema, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, hata ikawa hakuna mtu aliyeinua kichwa chake; lakini hawa wamekuja kuzifukuza, kuziangusha pembe za mataifa, walioinua pembe yao juu ya nchi ya Yuda, ili kuwatawanya watu wake.
Zekaria 1:1-21 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Katika mwezi wa nane, mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, BWANA amewakasirikia sana baba zenu. Basi, uwaambie, BWANA wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema BWANA wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunisikiliza, asema BWANA. Je! Baba zenu wako wapi? Nao manabii je! Waishi milele? Lakini maneno yangu, na amri zangu nilizowaagiza hao manabii, watumishi wangu, je! Hazikuwapata baba zenu? Nao wakageuka na kusema, Vile vile kama BWANA wa majeshi alivyoazimia kututenda, sawasawa na njia zetu, na sawasawa na matendo yetu, ndivyo alivyotutenda. Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, Naliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe. Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonyesha ni nini hawa. Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio BWANA aliowatuma, waende huko na huko duniani. Nao wakamjibu yule malaika wa BWANA aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huko na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe. Ndipo yule malaika wa BWANA akajibu, akasema, Ee BWANA wa majeshi, hata lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini? Naye BWANA akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja. Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana. Nami ninawakasirikia sana mataifa wanaokaa hali ya raha; kwa maana mimi sikukasirika ila kidogo tu, na wao waliyahimiza mateso. Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema BWANA wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu. Piga kelele tena, na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Miji yangu kwa kufanikiwa itaenezwa huko na huko tena; naye BWANA ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena. Nami nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, pembe nne. Nami nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Nini hizi? Naye akanijibu, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, na Israeli, na Yerusalemu. Kisha BWANA akanionyesha wafua chuma wanne. Ndipo nikauliza Hawa wanakuja kufanya nini? Akasema kwamba, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, hata ikawa hakuna mtu aliyeinua kichwa chake; lakini hawa wamekuja kuzifukuza, kuziangusha pembe za mataifa, walioinua pembe yao juu ya nchi ya Yuda, ili kuwatawanya watu wake.
Zekaria 1:1-21 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Katika mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kusema: “Mwenyezi Mungu aliwakasirikia sana baba zako wa zamani. Kwa hiyo waambie watu: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nirudieni mimi,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nami nitawarudia ninyi,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Msiwe kama baba zenu, ambao manabii waliotangulia waliwatangazia: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Geukeni, mziache njia zenu mbaya na matendo yenu maovu.’ Lakini hawakunisikiliza wala kufuata maelekezo yangu, asema Mwenyezi Mungu. Wako wapi baba zako sasa? Nao manabii, je, wanaishi milele? Je, maneno yangu na amri zangu nilizowaagiza manabii watumishi wangu, hayakuwapata baba zenu? “Kisha walitubu na kusema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ametutenda sawasawa na njia zetu na matendo yetu yalivyostahili, kama alivyokusudia kufanya.’ ” Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido. Wakati wa usiku nilipata maono, na tazama, mbele yangu palikuwa na mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia, na weupe. Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?” Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonesha kuwa ni nini.” Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewatuma waende duniani kote.” Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa Mwenyezi Mungu, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.” Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akasema, “Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, utazuia hadi lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?” Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami. Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni, lakini nimeyakasirikia sana mataifa yanayojisikia kuwa yako salama. Nilikuwa nimewakasirikia Israeli kidogo tu, lakini mataifa hayo yaliwazidishia maafa.’ “Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Nitairudia Yerusalemu kwa rehema na huko nyumba yangu itajengwa tena. Nayo kamba ya kupimia itanyooshwa juu ya Yerusalemu,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na Mwenyezi Mungu atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’ ” Kisha nikatazama juu, na pale mbele yangu nikaona pembe nne! Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Ni nini hizi?” Akanijibu, “Hizi ni zile pembe zilizowatawanya Yuda, Israeli na Yerusalemu.” Kisha Mwenyezi Mungu akanionesha mafundi wanne. Nikauliza, “Hawa wanakuja kufanya nini?” Akanijibu, “Hizi ndizo pembe zilizowatawanya Yuda ili asiwepo atakayeweza kuinua kichwa chake, lakini mafundi wamekuja kuzitia hofu na kuzitupa chini hizi pembe za mataifa ambayo yaliinua pembe zao dhidi ya nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”