Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 1:1-21

Zekaria 1:1-21 SRUV

Katika mwezi wa nane, mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, BWANA amewakasirikia sana baba zenu. Basi, uwaambie, BWANA wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema BWANA wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema BWANA wa majeshi. Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, BWANA wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunitii, asema BWANA. Je, Baba zenu wako wapi? Je, manabii nao wanaishi milele? Lakini maneno yangu, na amri zangu nilizowaagiza hao manabii, watumishi wangu, je, Hazikuwapata baba zenu? Nao wakatubu na kusema, BWANA wa majeshi ametutenda kulingana na njia zetu, na matendo yetu, kama alivyokusudia kutenda. Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la BWANA lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema, Niliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya miti ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe. Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonesha ni nini hawa. Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio BWANA aliowatuma, waende huku na huko duniani. Nao wakamjibu yule malaika wa BWANA aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huku na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe. Ndipo yule malaika wa BWANA akajibu, akasema, Ee BWANA wa majeshi, hadi lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini? Naye BWANA akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja. Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana. Nami ninayakasirikia sana mataifa yanayostarehe; kwa maana mimi nilikuwa nimekasirika kidogo tu, nao wakayazidisha maafa. Kwa sababu hiyo BWANA asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema BWANA wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu. Piga kelele tena, na kusema, BWANA wa majeshi asema hivi, Miji yangu itajawa na ufanisi tena; naye BWANA ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena. Nami nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, pembe nne. Nami nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Nini hizi? Naye akanijibu, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, na Israeli, na Yerusalemu. Kisha BWANA akanionesha wafua chuma wanne. Ndipo nikauliza, Hawa wanakuja kufanya nini? Akasema, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, hata ikawa hakuna mtu aliyeinua kichwa chake; lakini hawa wamekuja kuzifukuza, kuziangusha pembe za mataifa, walioinua pembe yao juu ya nchi ya Yuda, ili kuwatawanya watu wake.

Soma Zekaria 1