Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Zekaria 1:1-21

Zekaria 1:1-21 NENO

Katika mwezi wa nane wa mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia, mwana wa Ido, kusema: “Mwenyezi Mungu aliwakasirikia sana baba zako wa zamani. Kwa hiyo waambie watu: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nirudieni mimi,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, ‘nami nitawarudia ninyi,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. Msiwe kama baba zenu, ambao manabii waliotangulia waliwatangazia: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Geukeni, mziache njia zenu mbaya na matendo yenu maovu.’ Lakini hawakunisikiliza wala kufuata maelekezo yangu, asema Mwenyezi Mungu. Wako wapi baba zako sasa? Nao manabii, je, wanaishi milele? Je, maneno yangu na amri zangu nilizowaagiza manabii watumishi wangu, hayakuwapata baba zenu? “Kisha walitubu na kusema, ‘Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni ametutenda sawasawa na njia zetu na matendo yetu yalivyostahili, kama alivyokusudia kufanya.’ ” Katika siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa utawala wa Dario, neno la Mwenyezi Mungu lilimjia nabii Zekaria mwana wa Berekia mwana wa Ido. Wakati wa usiku nilipata maono, na tazama, mbele yangu palikuwa na mtu akiendesha farasi mwekundu! Alikuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi kwenye bonde. Nyuma yake walikuwepo farasi wekundu, wa kikahawia, na weupe. Nikauliza, “Hivi ni vitu gani bwana wangu?” Malaika aliyekuwa akizungumza na mimi akanijibu, “Nitakuonesha kuwa ni nini.” Kisha yule mtu aliyesimama katikati ya miti ya mihadasi akaeleza, “Ni wale ambao Mwenyezi Mungu amewatuma waende duniani kote.” Nao wakatoa taarifa kwa yule malaika wa Mwenyezi Mungu, aliyekuwa amesimama katikati ya miti ya mihadasi, “Tumepita duniani kote na kukuta ulimwengu wote umepumzika kwa amani.” Kisha malaika wa Mwenyezi Mungu akasema, “Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni, utazuia hadi lini rehema kutoka Yerusalemu na miji ya Yuda, ambayo umeikasirikia kwa miaka hii sabini?” Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akazungumza maneno ya upole na ya kufariji kwa malaika aliyezungumza nami. Kisha malaika yule aliyekuwa akizungumza nami akasema, “Tangaza neno hili: Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Nina wivu sana kwa ajili ya Yerusalemu na Sayuni, lakini nimeyakasirikia sana mataifa yanayojisikia kuwa yako salama. Nilikuwa nimewakasirikia Israeli kidogo tu, lakini mataifa hayo yaliwazidishia maafa.’ “Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: ‘Nitairudia Yerusalemu kwa rehema na huko nyumba yangu itajengwa tena. Nayo kamba ya kupimia itanyooshwa juu ya Yerusalemu,’ asema Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni. “Endelea kutangaza zaidi kwamba: Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni: ‘Miji yangu itafurika tena ustawi na Mwenyezi Mungu atamfariji tena Sayuni na kumchagua Yerusalemu.’ ” Kisha nikatazama juu, na pale mbele yangu nikaona pembe nne! Nikamuuliza yule malaika aliyekuwa akizungumza nami, “Ni nini hizi?” Akanijibu, “Hizi ni zile pembe zilizowatawanya Yuda, Israeli na Yerusalemu.” Kisha Mwenyezi Mungu akanionesha mafundi wanne. Nikauliza, “Hawa wanakuja kufanya nini?” Akanijibu, “Hizi ndizo pembe zilizowatawanya Yuda ili asiwepo atakayeweza kuinua kichwa chake, lakini mafundi wamekuja kuzitia hofu na kuzitupa chini hizi pembe za mataifa ambayo yaliinua pembe zao dhidi ya nchi ya Yuda na kuwatawanya watu wake.”