Zaburi 147:1-9
Zaburi 147:1-9 Biblia Habari Njema (BHN)
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa. Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia.
Zaburi 147:1-9 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu sifa, Maana ni mwenye fadhili, na anastahili kuimbiwa sifa. BWANA ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli. Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuyaganga majeraha yao. Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka. BWANA huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri. Mwimbieni BWANA kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi. Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuichipusha nyasi milimani. Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao.
Zaburi 147:1-9 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri. BWANA ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli. Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuziganga jeraha zao. Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka. BWANA huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri. Mwimbieni BWANA kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi. Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuyameesha majani milimani. Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao.
Zaburi 147:1-9 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Msifuni BWANA. Tazama jinsi ilivyo vyema kumwimbia Mungu wetu sifa, jinsi inavyopendeza na kustahili kumsifu yeye! BWANA hujenga Yerusalemu, huwakusanya Israeli walio uhamishoni. Anawaponya waliovunjika mioyo na kuvifunga vidonda vyao. Huzihesabu nyota na huipa kila moja jina lake. Bwana wetu ni mkuu na mwenye uwezo mwingi, ufahamu wake hauna kikomo. BWANA huwahifadhi wanyenyekevu lakini huwashusha waovu mpaka mavumbini. Mwimbieni BWANA kwa shukrani, mpigieni Mungu wetu kinubi. Yeye huzifunika anga kwa mawingu, huinyeshea ardhi mvua, na kuzifanya nyasi kuota juu ya vilima. Huwapa chakula mifugo na pia makinda ya kunguru yanapolia.