Zaburi 147:1-9
Zaburi 147:1-9 SRUV
Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu sifa, Maana ni mwenye fadhili, na anastahili kuimbiwa sifa. BWANA ndiye aijengaye Yerusalemu, Huwakusanya waliotawanyika wa Israeli. Huwaponya waliopondeka moyo, Na kuyaganga majeraha yao. Huihesabu idadi ya nyota, Huzipa zote majina. Bwana wetu ni mkuu na mwingi wa nguvu, Akili zake hazina mpaka. BWANA huwategemeza wenye upole, Huwaangusha chini wenye jeuri. Mwimbieni BWANA kwa kushukuru, Mwimbieni Mungu wetu kwa kinubi. Huzifunika mbingu kwa mawingu, Huitengenezea nchi mvua, Na kuichipusha nyasi milimani. Humpa mnyama chakula chake, Wana-kunguru waliao.