Zaburi 147:1-9
Zaburi 147:1-9 BHN
Msifuni Mwenyezi-Mungu! Jinsi gani ilivyo vizuri kumwimbia sifa Mungu wetu! Yeye ni mwema na astahili kuimbiwa sifa. Mwenyezi-Mungu anajenga tena mji wa Yerusalemu; anawarudisha Waisraeli waliokuwa uhamishoni. Anawaponya waliovunjika moyo; na kuwatibu majeraha yao. Anaamua idadi itakayokuwako ya nyota, na kuzipa zote majina yao. Bwana wetu ni mkuu, ana nguvu nyingi; maarifa yake hayana kipimo. Mwenyezi-Mungu huwakweza wanyenyekevu, lakini huwatupa waovu mavumbini. Mwimbieni Mwenyezi-Mungu nyimbo za shukrani, mpigieni kinubi Mungu wetu! Yeye hulifunika anga kwa mawingu, huitengenezea nchi mvua, na kuchipusha nyasi vilimani. Huwapa wanyama chakula chao, na kuwalisha makinda ya kunguru yanapolia.