Zaburi 13:1-6
Zaburi 13:1-6 Biblia Habari Njema (BHN)
Mpaka lini ee Mwenyezi-Mungu, utanisahau? Je, utanisahau mpaka milele? Mpaka lini utanificha uso wako? Nitakuwa na wasiwasi rohoni hadi lini, na sikitiko moyoni siku hata siku? Hadi lini adui zangu watafurahia taabu zangu? Uniangalie na kunijibu, ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu. Uyaangazie macho yangu, nisipatwe na usingizi wa kifo. Usiwaache maadui zangu waseme: “Tumemweza huyu!” Watesi wangu wasije wakafurahia kuanguka kwangu. Lakini mimi nazitumainia fadhili zako; moyo wangu na ufurahie wokovu wako. Nitakuimbia wewe, ee Mwenyezi-Mungu, kwa ukarimu mwingi ulionitendea!
Zaburi 13:1-6 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ee BWANA, utanisahau hadi lini, hata milele? Hadi lini utanificha uso wako? Nitakuwa na wasiwasi rohoni mwangu hadi lini, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Adui yangu atatukuka juu yangu hadi lini? Ee BWANA, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti. Adui yangu asije akasema, Nimemshinda; Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa. Lakini mimi nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako. Naam, nitamwimbia BWANA, Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu.
Zaburi 13:1-6 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ee BWANA, hata lini utanisahau, hata milele? Hata lini utanificha uso wako? Hata lini nifanye mashauri nafsini mwangu, Nikihuzunika moyoni mchana kutwa? Hata lini adui yangu atukuke juu yangu? Ee BWANA, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti. Adui yangu asije akasema, Nimemshinda; Watesi wangu wasifurahi ninapoondoshwa. Nami nimezitumainia fadhili zako; Moyo wangu na uufurahie wokovu wako. Naam, nimwimbie BWANA, Kwa kuwa amenitendea kwa ukarimu.
Zaburi 13:1-6 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Mpaka lini, Ee BWANA? Je, utanisahau milele? Utanificha uso wako mpaka lini? Nitapambana na mawazo yangu mpaka lini, na kila siku kuwa na majonzi moyoni mwangu? Adui zangu watanishinda mpaka lini? Nitazame, unijibu, Ee BWANA Mungu wangu. Yatie nuru macho yangu, ama sivyo nitalala usingizi wa mauti. Adui yangu atasema, “Nimemshinda,” nao adui zangu watashangilia nitakapoanguka. Lakini ninategemea upendo wako usiokoma; moyo wangu unashangilia katika wokovu wako. Nitamwimbia BWANA, kwa kuwa amekuwa mwema kwangu.