Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 7:1-10

Mika 7:1-10 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Ole wangu! Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa joto, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza. Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yao ni hodari kwa kutenda maovu; afisa na hakimu wanataka rushwa, mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja. Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao. Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe. Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu. Nitaivumilia ghadhabu ya BWANA, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea shutuma yangu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake. Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi BWANA, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu.

Shirikisha
Soma Mika 7

Mika 7:1-10 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Taabu gani hii niliyo nayo! Nimefanana na yule akusanyaye matunda ya kiangazi, aokotaye masazo baada ya kuvunwa shamba la mizabibu; hakuna kishada chenye matunda ya kula, hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani. Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi; hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki. Watu wote wanavizia kumwaga damu, kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya, mtawala anadai zawadi, hakimu anapokea rushwa, wenye nguvu wanaamuru wanachotaka: wote wanafanya shauri baya pamoja. Aliye mwema kupita wote kati yao ni kama mchongoma, anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao ni mbaya kuliko uzio wa miiba. Siku ya walinzi wako imewadia, siku atakayokutembelea Mungu. Sasa ni wakati wao wa kuchanganyikiwa. Usimtumaini jirani; usiweke matumaini kwa rafiki. Hata kwa yule alalaye kifuani mwako uwe mwangalifu kwa maneno yako. Kwa kuwa mwana humdharau baba yake, naye binti huinuka dhidi ya mama yake, mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake: adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa. Lakini mimi, namtazama BWANA kwa matumaini, namngoja Mungu Mwokozi wangu; Mungu wangu atanisikia mimi. Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu! Ingawa nimeanguka, nitainuka. Japo ninaketi gizani, BWANA atakuwa nuru yangu. Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake, nitabeba ghadhabu ya BWANA, mpaka atakaponitetea shauri langu na kuithibitisha haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaiona haki yake. Kisha adui yangu ataliona naye atafunikwa na aibu, yule aliyeniambia, “Yu wapi BWANA Mungu wako?” Macho yangu yataona kuanguka kwake, hata sasa atakanyagwa chini ya mguu kama tope barabarani.

Shirikisha
Soma Mika 7

Mika 7:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

Ole wangu! Hali ilivyo ni kama baada ya mavuno; hakuna tini za mwanzoni ninazotamani. Ni kama wakati wa kuchuma zabibu hakuna hata shada moja la zabibu la kula! Hakuna mcha Mungu aliyebaki nchini, hakuna mtu yeyote mnyofu miongoni mwa watu. Kila mmoja anavizia kumwaga damu; kila mmoja anamwinda mwenzake amnase. Wote ni mabingwa wa kutenda maovu; viongozi na mahakimu hutaka rushwa. Wakubwa huonesha wazi nia zao mbaya, na kufanya hila kuzitekeleza. Mwema zaidi kati yao hutaabisha kama mbigili, aliye mnyofu zaidi ni kama ua wa miiba. Siku iliyongojewa ya adhabu yao imefika. Na sasa mahangaiko yamewakumba. Usimwamini mwenzako, wala usimtumainie rafiki yako. Chunga unachosema kwa mdomo wako, hata na mke wako wewe mwenyewe. Maana, mtoto wa kiume anamdharau baba yake; mtoto wa kike anashindana na mama yake, mke wa mwana anapingana na mama mkwe wake. Maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. Lakini mimi namtumainia Mwenyezi-Mungu, namtazamia Mungu mwenye kuniokoa; Mungu wangu atanisikiliza. Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena; Nikiwa gizani, Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu. Kwa vile nimemkosea Mwenyezi-Mungu, sina budi kuvumilia ghadhabu yake, mpaka atakapotetea kisa changu na kunijalia haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaona akithibitisha haki. Hapo adui yangu ataona hayo naye atajaa aibu; maana aliniambia: “Wapi basi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako?” Mimi mwenyewe nitamwona adui akianguka; atakanyagwakanyagwa chini kama tope la njiani.

Shirikisha
Soma Mika 7

Mika 7:1-10 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Ole wangu! Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa hari, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza. Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yao inayashika mabaya wayatende kwa bidii; mtu mkuu aomba rushwa, kadhi yu tayari kuipokea; mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja. Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao. Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe. Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu. Nitaivumilia ghadhabu ya BWANA, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea teto langu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake. Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi BWANA, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu.

Shirikisha
Soma Mika 7