Mika 7:1-10
Mika 7:1-10 SRUV
Ole wangu! Maana mimi ni kama hapo walipokwisha kuyachuma matunda ya wakati wa joto, kama zabibu zichumwazo baada ya mavuno; hapana shada la kuliwa; roho yangu inatamani tini iivayo kwanza. Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yao ni hodari kwa kutenda maovu; afisa na hakimu wanataka rushwa, mtu mkubwa hunena madhara yaliyomo rohoni mwake; hivyo ndivyo wayafumavyo hayo pamoja. Mtu aliye mwema miongoni mwao ni kama mbigili; mtu aliye mwenye adili miongoni mwao ni mbaya kuliko boma la michongoma; hiyo siku ya walinzi wako, yaani, siku ya kujiliwa kwako, imefika; sasa kutatokea kufadhaika kwao. Msimwamini rafiki, msimwekee kiongozi tumaini; ilinde milango ya midomo ya kinywa chako ili mkeo alalaye kifuani mwako asijue habari. Kwa maana mwana humwaibisha babaye, na binti huondoka ashindane na mamaye; na mwanamke aliyeolewa hushindana na mavyaaye; adui za mtu ni watu wa nyumbani mwake mwenyewe. Lakini mimi, nitamtazamia BWANA; nitamngojea Mungu wa wokovu wangu; Mungu wangu atanisikia. Usifurahi juu yangu, Ee adui yangu; niangukapo, nitasimama tena; nikaapo gizani, BWANA atakuwa nuru kwangu. Nitaivumilia ghadhabu ya BWANA, kwa kuwa nimemwasi; hata atakaponitetea shutuma yangu, na kunifanyia hukumu; atanileta nje kwenye nuru, nami nitaiona haki yake. Ndipo adui yangu ataliona jambo hilo, na aibu itamfunika, yeye aliyeniambia, Yuko wapi BWANA, Mungu wako? Macho yangu yatamtazama; sasa atakanyagwa kama matope ya njia kuu.