Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mika 7:1-10

Mika 7:1-10 NEN

Taabu gani hii niliyo nayo! Nimefanana na yule akusanyaye matunda ya kiangazi, aokotaye masazo baada ya kuvunwa shamba la mizabibu; hakuna kishada chenye matunda ya kula, hakuna hata ile tini ya mwanzoni ninayoitamani. Wanaomcha Mungu wameondolewa kutoka nchi; hakuna mtu mnyofu hata mmoja aliyebaki. Watu wote wanavizia kumwaga damu, kila mmoja anamwinda ndugu yake kwa wavu. Mikono yote miwili ni hodari katika kufanya ubaya, mtawala anadai zawadi, hakimu anapokea rushwa, wenye nguvu wanaamuru wanachotaka: wote wanafanya shauri baya pamoja. Aliye mwema kupita wote kati yao ni kama mchongoma, anayeonekana mnyofu zaidi miongoni mwao ni mbaya kuliko uzio wa miiba. Siku ya walinzi wako imewadia, siku atakayokutembelea Mungu. Sasa ni wakati wao wa kuchanganyikiwa. Usimtumaini jirani; usiweke matumaini kwa rafiki. Hata kwa yule alalaye kifuani mwako uwe mwangalifu kwa maneno yako. Kwa kuwa mwana humdharau baba yake, naye binti huinuka dhidi ya mama yake, mkwe kuwa kinyume na mama mkwe wake: adui wa mtu ni wale wa nyumbani mwake hasa. Lakini mimi, namtazama BWANA kwa matumaini, namngoja Mungu Mwokozi wangu; Mungu wangu atanisikia mimi. Usifurahie msiba wangu, ee adui yangu! Ingawa nimeanguka, nitainuka. Japo ninaketi gizani, BWANA atakuwa nuru yangu. Kwa sababu nimetenda dhambi dhidi yake, nitabeba ghadhabu ya BWANA, mpaka atakaponitetea shauri langu na kuithibitisha haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaiona haki yake. Kisha adui yangu ataliona naye atafunikwa na aibu, yule aliyeniambia, “Yu wapi BWANA Mungu wako?” Macho yangu yataona kuanguka kwake, hata sasa atakanyagwa chini ya mguu kama tope barabarani.