Mika 7:1-10
Mika 7:1-10 BHN
Ole wangu! Hali ilivyo ni kama baada ya mavuno; hakuna tini za mwanzoni ninazotamani. Ni kama wakati wa kuchuma zabibu hakuna hata shada moja la zabibu la kula! Hakuna mcha Mungu aliyebaki nchini, hakuna mtu yeyote mnyofu miongoni mwa watu. Kila mmoja anavizia kumwaga damu; kila mmoja anamwinda mwenzake amnase. Wote ni mabingwa wa kutenda maovu; viongozi na mahakimu hutaka rushwa. Wakubwa huonesha wazi nia zao mbaya, na kufanya hila kuzitekeleza. Mwema zaidi kati yao hutaabisha kama mbigili, aliye mnyofu zaidi ni kama ua wa miiba. Siku iliyongojewa ya adhabu yao imefika. Na sasa mahangaiko yamewakumba. Usimwamini mwenzako, wala usimtumainie rafiki yako. Chunga unachosema kwa mdomo wako, hata na mke wako wewe mwenyewe. Maana, mtoto wa kiume anamdharau baba yake; mtoto wa kike anashindana na mama yake, mke wa mwana anapingana na mama mkwe wake. Maadui wa mtu ni watu wa nyumbani mwake. Lakini mimi namtumainia Mwenyezi-Mungu, namtazamia Mungu mwenye kuniokoa; Mungu wangu atanisikiliza. Usifurahie maafa yangu ewe adui yangu! Nikianguka, nitainuka tena; Nikiwa gizani, Mwenyezi-Mungu ni mwanga wangu. Kwa vile nimemkosea Mwenyezi-Mungu, sina budi kuvumilia ghadhabu yake, mpaka atakapotetea kisa changu na kunijalia haki yangu. Atanileta nje kwenye mwanga, nami nitaona akithibitisha haki. Hapo adui yangu ataona hayo naye atajaa aibu; maana aliniambia: “Wapi basi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako?” Mimi mwenyewe nitamwona adui akianguka; atakanyagwakanyagwa chini kama tope la njiani.