Luka 7:11-17
Luka 7:11-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake na kundi kubwa la watu waliandamana naye. Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya mwanamume mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama. Bwana alipomwona mama huyo akamwonea huruma, akamwambia, “Usilie.” Kisha, akaenda akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wamelichukua wakasimama. Halafu akasema, “Kijana! Nakuamuru, amka!” Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizo zikaenea kote katika Yudea na katika nchi za jirani.
Luka 7:11-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Baadaye kidogo alikwenda mpaka katika mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wengi mjini walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea kote katika Yudea yote, na katika nchi zote za karibu.
Luka 7:11-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Baadaye kidogo alikwenda mpaka mji mmoja uitwao Naini, na wanafunzi wake walifuatana naye pamoja na mkutano mkubwa. Na alipolikaribia lango la mji, hapo palikuwa na maiti anachukuliwa nje, ni mwana pekee wa mamaye ambaye ni mjane, na watu wa mjini wengi walikuwa pamoja naye. Bwana alipomwona alimwonea huruma, akamwambia, Usilie. Akakaribia, akaligusa jeneza; wale waliokuwa wakilichukua wakasimama. Akasema, Kijana, nakuambia, Inuka. Yule maiti akainuka, akaketi, akaanza kusema. Akampa mama yake. Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake. Habari hii yake ikaenea katika Uyahudi wote, na katika nchi zote za kando kando.
Luka 7:11-17 Neno: Maandiko Matakatifu 2024 (NENO)
Baadaye kidogo, Isa alienda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walienda pamoja naye. Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mwanamke. Bwana Isa alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.” Kisha akalikaribia jeneza, akaligusa. Nao wale waliokuwa wamelibeba wakasimama. Akasema, “Kijana, nakuambia, inuka.” Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Isa akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizi za mambo aliyoyafanya Isa zikaenea Yudea yote na sehemu zote za jirani.