Luka 7:11-17
Luka 7:11-17 BHN
Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja uitwao Naini, na wafuasi wake na kundi kubwa la watu waliandamana naye. Basi, alipokuwa anakaribia lango la mji, walitokea watu wamebeba maiti ya mwanamume mmoja, mtoto wa pekee wa mama mjane. Watu wengi wa mji ule walikuwa pamoja na huyo mama. Bwana alipomwona mama huyo akamwonea huruma, akamwambia, “Usilie.” Kisha, akaenda akaligusa lile jeneza, na wale waliokuwa wamelichukua wakasimama. Halafu akasema, “Kijana! Nakuamuru, amka!” Yule aliyekufa akaketi, akaanza kuongea. Na Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Watu wote walishikwa na hofu, wakawa wanamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea kati yetu. Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.” Habari hizo zikaenea kote katika Yudea na katika nchi za jirani.