Yobu 30:1-15
Yobu 30:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)
“Lakini sasa watu wananidhihaki, tena watu walio wadogo kuliko mimi; watu ambao baba zao niliwaona hawafai hata kuwaangalia mbwa wangu wakilinda kondoo. Ningepata faida gani mikononi mwao, watu ambao nguvu zao zilikuwa zimewaishia? Katika ufukara na njaa kali walitafutatafuta cha kutafuna nyikani sehemu tupu zisizokuwa na chakula. Walichuma mimea jangwani na majani msituni wakala, walikula hata mizizi ya mti wa mfagio. Walifukuzwa mbali na watu, watu waliwapigia kelele kama wezi. Iliwapasa kutafuta usalama mapangoni, kwenye mashimo ardhini na miambani. Huko vichakani walilia kama wanyama, walikusanyika pamoja chini ya upupu. Walikuwa wapumbavu wakuu na mabaradhuli ambao walilazimika kufukuzwa nchini kwa kiboko. “Na sasa wamenitungia wimbo wa kunizomea, nimekuwa kitu cha dhihaka kwao. Wananichukia na kuniepa; wakiniona tu wanatema mate. Kwa kuwa Mungu amenidhoofisha na kuniaibisha, wamekuwa huru kunitendea wapendavyo. Genge la watu lainuka kunishtaki likitafuta kuniangusha kwa kunitegea. Linanishambulia ili niangamie. Watu hao hukata njia yangu huchochea balaa yangu, na hapana mtu wa kuwazuia. Wanakuja kama kwenye ufa mkubwa, na baada ya shambulio wanasonga mbele. Hofu kuu imenishika; hadhi yangu imetoweka kama kwa upepo, na ufanisi wangu umepita kama wingu.
Yobu 30:1-15 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Lakini sasa hao walio wadogo wangu hunifanyia mzaha, Ambao baba zao ningewadharau hata kuwasimamia mbwa wa kundi langu. Naam, uwezo wa mikono yao utanifaa nini? Watu ambao nguvu zao zimekoma. Wamekonda kwa uhitaji na njaa; Huguguna nchi kavu, penye giza la ukiwa na uharibifu. Hung'oa mboga ya chumvi kwenye kichaka; Na mizizi ya mretemu ni chakula chao. Hufukuzwa watoke kati ya watu; Huwapigia kelele kama kumpigia mwizi. Lazima hukaa katika mianya ya mabonde, Katika mashimo ya nchi na ya majabali. Hulia kama punda vichakani; Hukusanyika chini ya upupu. Wao ni wana wa wapumbavu, naam, watoto wa wahuni; Walifukuzwa kwa mijeledi watoke katika nchi. Na sasa mimi nimekuwa wimbo wao, Naam, nimekuwa simo kwao. Wao hunichukia, na kujitenga nami, Hawaachi kunitemea mate usoni. Kwani ameilegeza kamba yake, na kunitesa, Wala hawajizuii tena mbele yangu. Kwa mkono wangu wa kulia huinuka kundi; Huisukuma miguu yangu kando, Na kunipandishia njia zao za uharibifu. Waiharibu njia yangu, Wauzidisha msiba wangu, Watu wasio na msaidizi. Wanijia kama wapitao katika ufa mpana; Katikati ya magofu wanishambulia. Vitisho vimenigeukia; Huifukuza heshima yangu kama upepo; Na kufanikiwa kwangu kumepita kama wingu.
Yobu 30:1-15 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Lakini sasa hao walio wadogo wangu hunifanyia mzaha, Ambao baba zao niliwadharau hata kuwaweka na mbwa wa kundi langu. Naam, uwezo wa mikono yao utanifaa nini? Watu ambao nguvu zao zimekoma. Wamekonda kwa uhitaji na njaa; Huguguna nchi kavu, penye giza la ukiwa na uharibifu. Hung’oa mboga ya chumvi kwenye kichaka; Na mizizi ya mretemu ni chakula chao. Hufukuzwa watoke kati ya watu; Huwapigia kelele kama kumpigia mwivi. Lazima hukaa katika mianya ya mabonde, Katika mashimo ya nchi na ya majabali. Hulia kama punda vichakani; Hukusanyika chini ya upupu. Wao ni wana wa wapumbavu, naam, watoto wa wahuni; Walifukuzwa kwa mijeledi watoke katika nchi. Na sasa mimi nimekuwa wimbo wao, Naam, nimekuwa simo kwao. Wao hunichukia, na kujitenga nami, Hawaachi kunitemea mate usoni. Kwani ameilegeza kamba yake, na kunitesa, Wala hawajizuii tena mbele yangu. Kwa mkono wangu wa kuume huinuka kundi; Huisukuma miguu yangu kando, Na kunipandishia njia zao za uharibifu. Waiharibu njia yangu, Wauzidisha msiba wangu, Watu wasio na msaidizi. Wanijilia kama wapitao katika ufa mpana; Katikati ya magofu wanishambulia. Vitisho vimenigeukia; Huifukuza heshima yangu kama upepo; Na kufanikiwa kwangu kumepita kama wingu.
Yobu 30:1-15 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Lakini sasa watu wadogo kwa umri kuniliko wananidhihaki, watu ambao baba zao ningekataa kwa dharau kuwaweka pamoja na mbwa wangu wa kulinda kondoo. Nguvu za mikono yao zingekuwa na faida gani kwangu, kwa kuwa nguvu zao zilikuwa zimewaishia? Wakiwa wamekonda kutokana na kupungukiwa na kwa njaa, walizurura usiku katika nchi kame iliyo ukiwa. Katika vichaka walikusanya mimea ya chumvi, nacho chakula chao kilikuwa mizizi ya mti wa mfagio. Walifukuzwa mbali na watu wao, wakipigiwa kelele kama wevi. Walilazimika kuishi katika mikondo ya vijito vilivyokauka, kwenye majabali na mahandaki. Kwenye vichaka walilia kama punda, na walijisongasonga pamoja kwenye vichaka. Wao ni watoto wa wapumbavu wenye asili ya ubaya, waliofukuzwa watoke katika nchi. “Nao sasa wana wao wananidhihaki katika nyimbo; nimekuwa kitu cha dhihaka kwao. Wananichukia sana na kujitenga nami, wala hawasiti kunitemea mate usoni. Sasa kwa kuwa Mungu ameilegeza kamba ya upinde wangu na kunitesa, wamekuwa huru kunitendea waonavyo. Kuume kwangu kundi linashambulia; wao huitegea miguu yangu tanzi, na kunizingira. Huizuia njia yangu, nao hufanikiwa katika kuniletea maafa, nami sina yeyote wa kunisaidia. Wananijia kama watu wapitao katika ufa mpana; katikati ya magofu huja na kunishambulia. Vitisho vimenifunika; heshima yangu imetoweshwa kama kwa upepo, salama yangu imetoweka kama wingu.