Yobu 30:1-15
Yobu 30:1-15 BHN
“Lakini sasa watu wananidhihaki, tena watu walio wadogo kuliko mimi; watu ambao baba zao niliwaona hawafai hata kuwaangalia mbwa wangu wakilinda kondoo. Ningepata faida gani mikononi mwao, watu ambao nguvu zao zilikuwa zimewaishia? Katika ufukara na njaa kali walitafutatafuta cha kutafuna nyikani sehemu tupu zisizokuwa na chakula. Walichuma mimea jangwani na majani msituni wakala, walikula hata mizizi ya mti wa mfagio. Walifukuzwa mbali na watu, watu waliwapigia kelele kama wezi. Iliwapasa kutafuta usalama mapangoni, kwenye mashimo ardhini na miambani. Huko vichakani walilia kama wanyama, walikusanyika pamoja chini ya upupu. Walikuwa wapumbavu wakuu na mabaradhuli ambao walilazimika kufukuzwa nchini kwa kiboko. “Na sasa wamenitungia wimbo wa kunizomea, nimekuwa kitu cha dhihaka kwao. Wananichukia na kuniepa; wakiniona tu wanatema mate. Kwa kuwa Mungu amenidhoofisha na kuniaibisha, wamekuwa huru kunitendea wapendavyo. Genge la watu lainuka kunishtaki likitafuta kuniangusha kwa kunitegea. Linanishambulia ili niangamie. Watu hao hukata njia yangu huchochea balaa yangu, na hapana mtu wa kuwazuia. Wanakuja kama kwenye ufa mkubwa, na baada ya shambulio wanasonga mbele. Hofu kuu imenishika; hadhi yangu imetoweka kama kwa upepo, na ufanisi wangu umepita kama wingu.