Yobu 19:1-20
Yobu 19:1-20 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini, Na kunivunjavunja kwa maneno? Mara kumi hizi mmenishutumu; Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu. Ingawaje nimekosa, Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe. Ikiwa mtajitukuza juu yangu, Na kufanya aibu yangu kuwa hoja juu yangu; Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake. Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu. Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na tumaini langu ameling'oa kama mti. Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu, Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake. Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao, Na kupiga kambi kuizunguka hema yangu. Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa. Watu wa ukoo wangu wamekoma, Na marafiki zangu niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Wageni nyumbani mwangu, na vijakazi wangu, wanihesabu kuwa mgeni. Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu. Pumzi zangu zimekuwa kinyaa kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu. Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Marafiki zangu wote wa dhati wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu.
Yobu 19:1-20 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndipo Ayubu akajibu: “Je, mtaendelea kunitesa mpaka lini, na kuniponda kwa maneno yenu? Mara kumi hizi mmenishutumu; bila aibu mnanishambulia. Kama ni kweli nimepotoka, kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe. Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu, na kutumia unyonge wangu dhidi yangu, basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya, naye amekokota wavu wake kunizunguka. “Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu; ingawa ninaomba msaada, hakuna haki. Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita; ameyafunika mapito yangu na giza. Amenivua heshima yangu, na kuniondolea taji kichwani pangu. Amenibomoa kila upande hadi nimeisha; amelingʼoa tegemeo langu kama mti. Hasira yake imewaka juu yangu; amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake. Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu; yamenizingira, yamepiga kambi kulizunguka hema langu. “Amewatenga ndugu zangu mbali nami; wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa. Watu wa jamaa yangu wamekwenda mbali; rafiki zangu wamenisahau. Wageni wangu na watumishi wangu wa kike wananiona kama mgeni; wananitazama kama mgeni. Namwita mtumishi wangu, wala haitiki, ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe. Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu; nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe. Hata watoto wadogo hunidhihaki; ninapojitokeza, hunifanyia mzaha. Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa; wale niwapendao wamekuwa kinyume nami. Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu; nimeponea nikiwa karibu kufa.
Yobu 19:1-20 Biblia Habari Njema (BHN)
Kisha Yobu akajibu: “Mtaendelea kunitesa mpaka lini, na kunivunjavunja kwa maneno? Mara hizi zote kumi mmenishutumu. Je, hamwoni aibu kunitendea vibaya? Hata kama ingekuwa nimekosa kweli, kosa langu lanihusu mimi mwenyewe. Mnaishusha hadhi yangu mpate kujikuza; mnanilaumu kwa kunyenyekezwa kwangu. Jueni kwamba Mungu amenitendea vibaya, na kuninasa katika wavu wake. Tazama napiga yowe: ‘Dhuluma!’ Lakini sijibiwi. Naita kwa sauti kubwa, lakini sipati haki yangu. Njia yangu ameiziba kwa ukuta ili nisipite amezitia giza njia zangu. Amenivua fahari yangu; ameiondoa taji yangu kichwani. Amenivunja pande zote, nami nimekwisha; tumaini langu amelingoa kama mti. Ameichochea ghadhabu yake dhidi yangu; ameniona kuwa kama adui yake. Majeshi yake yanijia kwa pamoja; yametengeneza njia ya kuja kwangu, yamepiga kambi kuizunguka nyumba yangu. Mungu amewaweka ndugu zangu mbali nami; rafiki zangu wakuu wamenitoroka kabisa. Jamaa zangu na marafiki hawanisaidii tena. Wageni nyumbani mwangu wamenisahau; watumishi wangu wa kike waniona kuwa mgeni. Mimi nimekuwa kwao mtu wasiyemjua. Namwita mtumishi wangu lakini haitikii, ninalazimika kumsihi sana kwa maneno. Nimekuwa kinyaa kwa mke wangu; chukizo kwa ndugu zangu mwenyewe. Hata watoto wadogo hunidharau, mara ninapojitokeza wao hunizomea. “Rafiki zangu wakuu wanachukizwa nami, wale niliokuwa nikiwapenda wamenipa kisogo. Mwili wangu umebakia tu mifupa na ngozi, nimeponea chupuchupu baada ya kupoteza yote.
Yobu 19:1-20 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini, Na kunivunja-vunja kwa maneno? Mara kumi hizi mmenishutumu; Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu. Ingawaje nimekosa, Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe. Kwamba mtajitukuza juu yangu, Na kunena juu yangu shutumu langu; Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake. Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu. Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na tumaini langu ameling’oa kama mti. Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu, Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake. Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao, Na kupiga marago kuizunguka hema yangu. Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa. Watu wa mbari yangu wamekoma, Na rafiki zangu niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Mimi ni mgeni machoni pao. Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu. Pumzi zangu ni kama za mgeni kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu. Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Wasiri wangu wote wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu.