Ayubu 19:1-20
Ayubu 19:1-20 SRUV
Ndipo Ayubu akajibu, na kusema, Je! Mtanichukiza nafsi yangu hata lini, Na kunivunjavunja kwa maneno? Mara kumi hizi mmenishutumu; Hamwoni haya kunifanyia mambo magumu. Ingawaje nimekosa, Kosa langu hukaa kwangu mwenyewe. Ikiwa mtajitukuza juu yangu, Na kufanya aibu yangu kuwa hoja juu yangu; Jueni basi kuwa Mungu amenipotosha, Na kunizingira kwa wavu wake. Tazama, nalia, Udhalimu, lakini sisikiwi; Naulilia msaada, wala hapana hukumu. Yeye ameiziba njia yangu nisipate kupita, Na kutia giza katika mapito yangu. Amenivua utukufu wangu, Na kuiondoa taji kichwani mwangu. Amenibomoa pande zote, nami nimetoweka; Na tumaini langu ameling'oa kama mti. Tena ameziwasha ghadhabu zake juu yangu, Akanihesabia kuwa mmoja katika watesi wake. Majeshi yake husongea pamoja, na kunipandishia njia yao, Na kupiga kambi kuizunguka hema yangu. Amewaweka ndugu zangu mbali nami, Na wanijuao wametengwa nami kabisa. Watu wa ukoo wangu wamekoma, Na marafiki zangu niwapendao wamenisahau. Wakaao nyumbani mwangu, na vijakazi vyangu, wanihesabu kuwa mgeni; Wageni nyumbani mwangu, na vijakazi wangu, wanihesabu kuwa mgeni. Namwita mtumishi wangu, wala haniitikii, Ingawa namsihi kwa kinywa changu. Pumzi zangu zimekuwa kinyaa kwa mke wangu, Nami ni machukizo kwa ndugu zangu. Hata watoto wadogo hunidharau; Nikiondoka, huninena. Marafiki zangu wote wa dhati wanichukia; Na hao niliowapenda wamenigeukia. Mfupa wangu unagandamana na ngozi yangu na nyama yangu, Nami nimeokoka na ngozi ya meno yangu tu.