Ayubu 19:1-20
Ayubu 19:1-20 NEN
Ndipo Ayubu akajibu: “Je, mtaendelea kunitesa mpaka lini, na kuniponda kwa maneno yenu? Mara kumi hizi mmenishutumu; bila aibu mnanishambulia. Kama ni kweli nimepotoka, kosa langu ninabaki kuhusika nalo mwenyewe. Kama kweli mngejitukuza wenyewe juu yangu, na kutumia unyonge wangu dhidi yangu, basi jueni kuwa Mungu amenitendea yaliyo mabaya, naye amekokota wavu wake kunizunguka. “Ingawa ninalia, ‘Nimetendewa mabaya!’ sipati jibu; ingawa ninaomba msaada, hakuna haki. Yeye ameizuia njia yangu hivyo siwezi kupita; ameyafunika mapito yangu na giza. Amenivua heshima yangu, na kuniondolea taji kichwani pangu. Amenibomoa kila upande hadi nimeisha; amelingʼoa tegemeo langu kama mti. Hasira yake imewaka juu yangu; amenihesabu kuwa miongoni mwa adui zake. Majeshi yake yananisogelea kwa nguvu; yamenizingira, yamepiga kambi kulizunguka hema langu. “Amewatenga ndugu zangu mbali nami; wale tunaojuana nao wamefarakana nami kabisa. Watu wa jamaa yangu wamekwenda mbali; rafiki zangu wamenisahau. Wageni wangu na watumishi wangu wa kike wananiona kama mgeni; wananitazama kama mgeni. Namwita mtumishi wangu, wala haitiki, ingawa namwomba kwa kinywa changu mwenyewe. Pumzi ya kinywa changu ni kinyaa kwa mke wangu; nimekuwa chukizo mno kwa ndugu zangu mwenyewe. Hata watoto wadogo hunidhihaki; ninapojitokeza, hunifanyia mzaha. Rafiki zangu wa moyoni wote wananichukia kabisa; wale niwapendao wamekuwa kinyume nami. Mimi nimebaki mifupa na ngozi tu; nimeponea nikiwa karibu kufa.