Isaya 62:6-12
Isaya 62:6-12 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapoufanya imara Yerusalemu, na kuufanya kuwa sifa duniani. BWANA ameapa kwa mkono wake wa kuume, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi. Lakini walioivuna, ndio watakaoila, na kumhimidi BWANA; na walioichuma, ndio watakaoinywa, ndani ya nyua za patakatifu pangu. Piteni, piteni, katika malango; Itengenezeni njia ya watu; Tutieni, tutieni barabara; toeni mawe yake; Twekeni bendera kwa ajili ya kabila za watu. Tazama, BWANA ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia, Mwambieni binti Sayuni, Tazama, wokovu wako unakuja; Tazama, thawabu yake i pamoja naye, Na malipo yake yako mbele zake. Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na BWANA; Nawe utaitwa, Aliyetafutwa, Mji usioachwa.
Isaya 62:6-12 Biblia Habari Njema (BHN)
“Juu ya kuta zako ee Yerusalemu nimeweka walinzi, usiku na mchana kamwe hawatakaa kimya.” Enyi mnaomkumbusha Mwenyezi-Mungu ahadi yake, msikae kimya; msimpe hata nafasi ya kupumzika, mpaka atakapousimika mji wa Yerusalemu, na kuufanya uwe fahari ulimwenguni kote. Mwenyezi-Mungu ameapa kwa mkono wake wa kulia, naam, ameapa kwa mkono wake wenye nguvu akisema: “Sitawapa tena maadui zako nafaka yako; wala wageni hawatakunywa tena divai yako ambayo umeitolea jasho. Bali nyinyi mliyoivuna nafaka hiyo, mtaila na kunitukuza mimi Mwenyezi-Mungu. Nyinyi mliochuma zabibu hizo, mtakunywa divai yake katika nyua zangu takatifu.” Wakazi wa Yerusalemu, tokeni, tokeni nje ya mji, watayarishieni njia watu wenu wanaorejea! Jengeni! Jengeni barabara na kuondoa mawe yote! Wekeni alama kwa ajili ya watu. Mwenyezi-Mungu ametangaza duniani kote, waambie watu wa Siyoni: “Mkombozi wenu anakuja, zawadi yake iko pamoja naye na tuzo lake liko mbele yake.” Nyinyi mtaitwa: “Watu Watakatifu”, “Watu waliokombolewa na Mwenyezi-Mungu.” Na Yerusalemu utaitwa: “Mji aupendao Mungu”, “Mji ambao Mungu hakuuacha.”
Isaya 62:6-12 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, Ee Yerusalemu; hawatanyamaza mchana wala usiku; ninyi wenye kumkumbusha BWANA, msiwe na kimya; wala msimwache akae kimya, mpaka atakapouimarisha Yerusalemu, na kuufanya usifike kote duniani. BWANA ameapa kwa mkono wake wa kulia, na kwa mkono wa nguvu zake, Hakika sitawapa adui zako nafaka yako tena kuwa chakula chao; wala wageni hawatakunywa divai yako, uliyoifanyia kazi. Lakini walioivuna, ndio watakaoila, na kumhimidi BWANA; na walioichuma, ndio watakaoinywa, ndani ya nyua za patakatifu pangu. Piteni, piteni, katika malango; Itengenezeni njia ya watu; Tutieni, tutieni barabara; toeni mawe yake; Twekeni bendera kwa ajili ya makabila ya watu. Tazama, BWANA ametangaza habari mpaka mwisho wa dunia, Mwambieni binti Sayuni, Tazama, wokovu wako unakuja; Tazama, thawabu yake iko pamoja naye, Na malipo yake yako mbele zake. Nao watawaita, Watu watakatifu, Waliokombolewa na BWANA; Nawe utaitwa, Aliyetafutwa, Mji usioachwa.
Isaya 62:6-12 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Nimeweka walinzi juu ya kuta zako, ee Yerusalemu, hawatanyamaza mchana wala usiku. Ninyi wenye kumwita BWANA, msitulie, msimwache apumzike hadi atakapoufanya imara Yerusalemu na kuufanya uwe sifa ya dunia. BWANA ameapa kwa mkono wake wa kuume na kwa mkono wake wenye nguvu: “Kamwe sitawapa tena adui zenu nafaka zenu kama chakula chao; kamwe wageni hawatakunywa tena divai mpya ambayo mmeitaabikia, lakini wale waivunao nafaka wataila na kumsifu BWANA, nao wale wakusanyao zabibu watainywa divai yake katika nyua za patakatifu pangu.” Piteni, piteni katika malango! Tengenezeni njia kwa ajili ya watu. Jengeni, jengeni njia kuu! Ondoeni mawe. Inueni bendera kwa ajili ya mataifa. BWANA ametoa tangazo mpaka miisho ya dunia: “Mwambie Binti Sayuni, ‘Tazama, mwokozi wako anakuja! Tazama ujira wake uko pamoja naye, na malipo yake yanafuatana naye!’ ” Wataitwa Watu Watakatifu, Waliokombolewa na BWANA; nawe utaitwa Aliyetafutwa, Mji Usioachwa Tena.