Hosea 9:10-17
Hosea 9:10-17 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Mimi nilimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami niliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza, msimu wake wa kwanza; lakini walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda. Naye Efraimu, utukufu wake utarukia mbali kama ndege, uzazi hautakuwako, wala aliye na mimba, wala achukuaye mimba. Wajapolea watoto wao, mimi nitawanyang'anya watoto wao, asisalie hata mtu mmoja; naam, ole wao! Nitakapoondoka na kuwaacha. Efraimu amepandwa mahali pazuri, kama nilivyoona Tiro; lakini Efraimu atamtolea mwuaji watoto wake. Wape, Ee BWANA; utawapa kitu gani? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na maziwa makavu. Uovu wao wote u katika Gilgali; maana huko niliwachukia; kwa sababu ya uovu wa matendo yao nitawafukuza watoke katika nyumba yangu; sitawapenda tena; wakuu wao wote ni waasi. Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana. Mungu wangu atawatupilia mbali, kwa sababu hawakumsikiliza; nao watakuwa watu wa kutangatanga kati ya mataifa.
Hosea 9:10-17 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Mimi nalimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami naliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza, wakati wake wa kwanza; lakini walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda. Naye Efraimu, utukufu wake utarukia mbali kama ndege, uzazi hautakuwako, wala aliye na mimba, wala achukuaye mimba. Wajapolea watoto wao, mimi nitawanyang’anya watoto wao, asisalie hata mtu mmoja; naam, ole wao! Nitakapoondoka na kuwaacha. Efraimu amepandwa mahali pazuri, kama nilivyoona Tiro; lakini Efraimu atamtolea mwuaji watoto wake. Wape, Ee BWANA; utawapa kitu gani? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na maziwa makavu. Uovu wao wote u katika Gilgali; maana huko naliwachukia; kwa sababu ya uovu wa matendo yao nitawafukuza watoke katika nyumba yangu; sitawapenda tena; wakuu wao wote ni waasi. Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana. Mungu wangu atawatupilia mbali, kwa sababu hawakumsikiliza; nao watakuwa watu wa kutanga-tanga kati ya mataifa.
Hosea 9:10-17 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
“Nilipompata Israeli, ilikuwa kama kupata zabibu jangwani; nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona matunda ya kwanza katika mtini. Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu kwa ile sanamu ya aibu, nao wakawa najisi kama kitu kile walichokipenda. Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege: hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba, hakuna kutunga mimba. Hata wakilea watoto, nitamuua kila mmoja. Ole wao nitakapowapiga kisogo! Nimemwona Efraimu, kama Tiro, aliyeoteshwa mahali pazuri. Lakini Efraimu wataleta watoto wao kwa mchinjaji.” Wape, Ee BWANA, je, utawapa nini? Wape matumbo ya kuharibu mimba na matiti yaliyokauka. “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, niliwachukia huko. Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, nitawafukuza katika nyumba yangu. Sitawapenda tena, viongozi wao wote ni waasi. Efraimu ameharibiwa, mzizi wao umenyauka, hawazai tunda. Hata kama watazaa watoto, nitawachinja watoto wao waliotunzwa vizuri.” Mungu wangu atawakataa kwa sababu hawakumtii; watakuwa watu wa kutangatanga miongoni mwa mataifa.
Hosea 9:10-17 Biblia Habari Njema (BHN)
Mwenyezi-Mungu asema: “Nilipowakuta Waisraeli walikuwa kama zabibu jangwani. Nilipowaona wazee wenu walikuwa bora kama tini za kwanza. Lakini mara walipofika huko Baal-peori, walijiweka wakfu kuabudu chukizo Baali, wakawa chukizo kama hicho walichokipenda. Fahari ya Efraimu itatoweka kama ndege; watoto hawatazaliwa tena, hakutakuwa na watoto wa kuzaliwa, wala hakutakuwa na kuchukuliwa mimba! Hata kama wakilea watoto, sitamwacha hai hata mmoja wao. Ole wao, nitakapowaacha peke yao!” Kama nilivyokwisha ona hapo kwanza, Efraimu alikuwa kama mtende mchanga penye konde zuri; lakini sasa Efraimu itamlazimu kuwapeleka watoto wake wauawe. Uwaadhibu watu hawa ee Mwenyezi-Mungu! Lakini utawaadhibu namna gani? Uwafanye wanawake wao kuwa tasa; uwafanye wakose maziwa ya kunyonyesha watoto wao! Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Uovu wao wote ulianzia Gilgali; huko ndiko nilipoanza kuwachukia. Kwa sababu ya uovu wa matendo yao, nitawafukuza nyumbani kwangu. Sitawapenda tena. Viongozi wao wote ni waasi. Watu wa Efraimu wamepigwa, wamekuwa kama mti wenye mzizi mkavu, hawatazaa watoto wowote. Hata kama wakizaa watoto, nitawaua watoto wao wawapendao.” Kwa vile wamekataa kumsikiliza, Mungu wangu atawatupa; wao watatangatanga kati ya mataifa.