Hosea 9:10-17
Hosea 9:10-17 NEN
“Nilipompata Israeli, ilikuwa kama kupata zabibu jangwani; nilipowaona baba zenu, ilikuwa kama kuona matunda ya kwanza katika mtini. Lakini walipofika Baal-Peori, walijiweka wakfu kwa ile sanamu ya aibu, nao wakawa najisi kama kitu kile walichokipenda. Utukufu wa Efraimu utaruka kama ndege: hakuna kuzaa, hakuna kuchukua mimba, hakuna kutunga mimba. Hata wakilea watoto, nitamuua kila mmoja. Ole wao nitakapowapiga kisogo! Nimemwona Efraimu, kama Tiro, aliyeoteshwa mahali pazuri. Lakini Efraimu wataleta watoto wao kwa mchinjaji.” Wape, Ee BWANA, je, utawapa nini? Wape matumbo ya kuharibu mimba na matiti yaliyokauka. “Kwa sababu ya uovu wao wote huko Gilgali, niliwachukia huko. Kwa sababu ya matendo yao ya dhambi, nitawafukuza katika nyumba yangu. Sitawapenda tena, viongozi wao wote ni waasi. Efraimu ameharibiwa, mzizi wao umenyauka, hawazai tunda. Hata kama watazaa watoto, nitawachinja watoto wao waliotunzwa vizuri.” Mungu wangu atawakataa kwa sababu hawakumtii; watakuwa watu wa kutangatanga miongoni mwa mataifa.