Hosea 9:10-17
Hosea 9:10-17 SRUV
Mimi nilimkuta Israeli kama zabibu nyikani; nami niliwaona baba zenu kama matunda ya mtini yaliyoiva kwanza, msimu wake wa kwanza; lakini walikwenda Baal-Peori, wakajiweka wakfu kwa kitu cha aibu, wakawa chukizo kama kitu kile walichokipenda. Naye Efraimu, utukufu wake utarukia mbali kama ndege, uzazi hautakuwako, wala aliye na mimba, wala achukuaye mimba. Wajapolea watoto wao, mimi nitawanyang'anya watoto wao, asisalie hata mtu mmoja; naam, ole wao! Nitakapoondoka na kuwaacha. Efraimu amepandwa mahali pazuri, kama nilivyoona Tiro; lakini Efraimu atamtolea mwuaji watoto wake. Wape, Ee BWANA; utawapa kitu gani? Wape tumbo lenye kuharibu mimba na maziwa makavu. Uovu wao wote u katika Gilgali; maana huko niliwachukia; kwa sababu ya uovu wa matendo yao nitawafukuza watoke katika nyumba yangu; sitawapenda tena; wakuu wao wote ni waasi. Efraimu amepigwa; mzizi wao umekauka; hawatazaa matunda; naam, wajapozaa, nitaliua tunda la tumbo lipendwalo sana. Mungu wangu atawatupilia mbali, kwa sababu hawakumsikiliza; nao watakuwa watu wa kutangatanga kati ya mataifa.