Hosea 9:10-17
Hosea 9:10-17 BHN
Mwenyezi-Mungu asema: “Nilipowakuta Waisraeli walikuwa kama zabibu jangwani. Nilipowaona wazee wenu walikuwa bora kama tini za kwanza. Lakini mara walipofika huko Baal-peori, walijiweka wakfu kuabudu chukizo Baali, wakawa chukizo kama hicho walichokipenda. Fahari ya Efraimu itatoweka kama ndege; watoto hawatazaliwa tena, hakutakuwa na watoto wa kuzaliwa, wala hakutakuwa na kuchukuliwa mimba! Hata kama wakilea watoto, sitamwacha hai hata mmoja wao. Ole wao, nitakapowaacha peke yao!” Kama nilivyokwisha ona hapo kwanza, Efraimu alikuwa kama mtende mchanga penye konde zuri; lakini sasa Efraimu itamlazimu kuwapeleka watoto wake wauawe. Uwaadhibu watu hawa ee Mwenyezi-Mungu! Lakini utawaadhibu namna gani? Uwafanye wanawake wao kuwa tasa; uwafanye wakose maziwa ya kunyonyesha watoto wao! Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Uovu wao wote ulianzia Gilgali; huko ndiko nilipoanza kuwachukia. Kwa sababu ya uovu wa matendo yao, nitawafukuza nyumbani kwangu. Sitawapenda tena. Viongozi wao wote ni waasi. Watu wa Efraimu wamepigwa, wamekuwa kama mti wenye mzizi mkavu, hawatazaa watoto wowote. Hata kama wakizaa watoto, nitawaua watoto wao wawapendao.” Kwa vile wamekataa kumsikiliza, Mungu wangu atawatupa; wao watatangatanga kati ya mataifa.