Waebrania 10:11-18
Waebrania 10:11-18 Biblia Habari Njema (BHN)
Kila kuhani Myahudi hutoa huduma yake ya ibada ya kila siku na kutoa tambiko zilezile mara nyingi, tambiko ambazo haziwezi kuondoa dhambi. Lakini Kristo alitoa tambiko moja kwa ajili ya dhambi, tambiko ifaayo milele, kisha, akaketi upande wa kulia wa Mungu, anangoja maadui zake wafanywe kama kibao chini ya miguu yake. Basi, kwa tambiko yake moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wote wale wanaotakaswa dhambi zao. Naye Roho Mtakatifu anatupa ushahidi wake. Kwanza anasema: “Hili ndilo agano nitakalofanya nao, siku zijazo, asema Bwana: Nitaweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika akilini mwao.” Kisha akaongeza kusema: “Sitakumbuka tena dhambi zao, wala vitendo vyao vya uhalifu.” Basi, dhambi zikisha ondolewa, hakutakuwa na haja tena ya kutoa tambiko za kuondoa dhambi.
Waebrania 10:11-18 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kulia wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika fikira zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
Waebrania 10:11-18 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu; tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema, Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo, Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa. Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
Waebrania 10:11-18 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake, kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa. Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema: “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika katika nia zao.” Kisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao sitakumbuka tena.” Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.