Waebrania 10:11-18
Waebrania 10:11-18 NEN
Kila kuhani husimama siku kwa siku akifanya huduma yake ya ibada, na kutoa tena na tena dhabihu zile zile ambazo haziwezi kamwe kuondoa dhambi. Lakini huyu kuhani akiisha kutoa dhabihu moja kwa ajili ya dhambi kwa wakati wote, aliketi mkono wa kuume wa Mungu. Tangu wakati huo anangoja mpaka adui zake wawekwe chini ya miguu yake, kwa sababu kwa dhabihu moja amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wote wanaotakaswa. Pia Roho Mtakatifu anatushuhudia kuhusu jambo hili. Kwanza anasema: “Hili ndilo Agano nitakalofanya nao baada ya siku hizo, asema Bwana. Nitaziweka sheria zangu mioyoni mwao, na kuziandika katika nia zao.” Kisha aongeza kusema: “Dhambi zao na kutokutii kwao sitakumbuka tena.” Basi haya yakiisha kusamehewa, hakuna tena dhabihu yoyote inayotolewa kwa ajili ya dhambi.