Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Waraka kwa Waebrania 10

10
Kafara ya Kristo inatosha
1 # Ebr 8:5; 7:19 Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wowote kuwakamilisha wakaribiao. 2Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi? 3#Law 16:21 Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka. 4Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. 5#Zab 40:6-8 Kwa hiyo alipokuja ulimwenguni, alisema,
Dhabihu na matoleo hukutaka,
Lakini mwili uliniwekea tayari;
6Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;
7Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la kitabu nimeandikiwa)
Niyafanye mapenzi yako, Mungu.
8Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), 9ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. 10#Ebr 9:12,28 Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu. 11#Kut 29:38 Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi. 12#Zab 110:1 Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kulia wa Mungu; 13tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake. 14Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa. 15Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema,
16 # Yer 31:33; Ebr 8:10 Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana,
Nitatia sheria zangu mioyoni mwao,
Na katika fikira zao nitaziandika;
ndipo anenapo,
17 # Yer 31:34; Ebr 8:12 Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa.
18Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.
Wito wa kuwa Wavumilivu
19 # Mt 27:51 Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, 20#Ebr 9:8 njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; 21#Zek 6:11; Hes 12:7 na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; 22#Law 8:30; Eze 36:25; Efe 5:26 na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi. 23#Ebr 4:14 Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; 24#Ebr 13:1 tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; 25#Ebr 3:13 wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri muonavyo siku ile kuwa inakaribia.
26 # Ebr 6:4-8; 1 Tim 2:4 Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi; 27#Isa 26:11 bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao. 28#Kum 17:6; 19:15; Hes 15:30; 35:30 Mtu aliyeidharau Sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu. 29#Kut 24:8; Ebr 2:3 Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema? 30#Kum 32:35-36; Zab 135:14; Rum 12:19 Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake. 31#Ebr 12:29 Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.
32 # Ebr 6:4 Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; 33#1 Kor 4:9 pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo. 34#Mt 6:20; 19:21,29 Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. 35#Ebr 11:6 Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu. 36#Ebr 6:12; Lk 21:19 Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.
37 # Hab 2:3-4; Isa 26:20; Lk 21:28; Yak 5:8 Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana,
Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.
38 # Rum 1:17; Gal 3:11 Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani;
Naye akisitasita, roho yangu haina furaha naye.
39Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha