Mwanzo 45:1-8
Mwanzo 45:1-8 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinipeleka mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo na kulima wala kuvuna. Mungu alinipeleka mbele yenu kuwahifadhia masazo katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionipeleka huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.
Mwanzo 45:1-8 Biblia Habari Njema (BHN)
Hapo Yosefu akashindwa kujizuia mbele ya wote walioandamana naye, akawaamuru watoke nje. Hivyo Yosefu alikuwa peke yake alipojitambulisha kwa ndugu zake. Lakini alilia kwa sauti kubwa hata Wamisri wakamsikia, hali kadhalika na watu wa jamaa ya Farao nao wakamsikia. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu. Je, baba yangu angali hai?” Lakini ndugu zake wakapigwa na bumbuazi mbele yake, hata wakashindwa kumjibu. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri. Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu. Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno. Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa. Kwa hiyo, si nyinyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Ndiye aliyenifanya kama baba kwa Farao, msimamizi wa nyumba yake yote na mtawala wa nchi yote ya Misri.
Mwanzo 45:1-8 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Hapo Yusufu hakuweza kujizuia mbele yao wote waliosimama karibu naye. Akapiga kelele, na kusema, Mwondoeni kila mtu mbele yangu. Wala hakusimama mtu pamoja naye, Yusufu alipojitambulisha kwa nduguze. Akapaza sauti yake akalia, nao Wamisri wakasikia. Watu wa nyumba ya Farao nao wakasikia. Yusufu akawaambia ndugu zake, Mimi ndimi Yusufu; baba yangu angali hai bado? Wala ndugu zake hawakuweza kumjibu, maana waliingiwa na hofu mbele yake. Yusufu akawaambia ndugu zake, Karibuni kwangu; basi, wakakaribia. Akasema, Mimi ni Yusufu, ndugu yenu, ambaye mliniuza kwenda Misri. Basi sasa, msihuzunike, wala msiudhike nafsi zenu, kwa kuniuza huku; maana Mungu alinituma mbele yenu kuhifadhi maisha ya watu. Maana miaka hii miwili njaa imekuwa katika nchi, na iko tena miaka mitano isiyo ya kulima wala kuvuna. Mungu alinituma mbele yenu kuwahifadhia mabaki katika nchi, na kuwaokoa ninyi kwa wokovu mkuu. Basi si ninyi mlionileta huku, ila Mungu; naye ameniweka kama baba kwa Farao, na bwana katika nyumba yake yote, na mtawala katika nchi yote ya Misri.
Mwanzo 45:1-8 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu yeyote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake. Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri! Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu. “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote.