Mwanzo 45:1-8
Mwanzo 45:1-8 NEN
Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu yeyote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake. Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake. Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimuuza Misri! Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi. Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna. Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu. “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote.