Mwanzo 45:1-8
Mwanzo 45:1-8 BHN
Hapo Yosefu akashindwa kujizuia mbele ya wote walioandamana naye, akawaamuru watoke nje. Hivyo Yosefu alikuwa peke yake alipojitambulisha kwa ndugu zake. Lakini alilia kwa sauti kubwa hata Wamisri wakamsikia, hali kadhalika na watu wa jamaa ya Farao nao wakamsikia. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu. Je, baba yangu angali hai?” Lakini ndugu zake wakapigwa na bumbuazi mbele yake, hata wakashindwa kumjibu. Yosefu akawaambia ndugu zake, “Tafadhali, sogeeni karibu nami.” Walipomkaribia, akawaambia, “Mimi ndiye ndugu yenu Yosefu, mliyemwuza Misri. Lakini sasa msifadhaike wala kujilaumu kwa kuniuza. Mungu ndiye aliyenileta huku niwatangulie, ili niyaokoe maisha ya watu. Huu ni mwaka wa pili tu wa njaa nchini, na bado kuna miaka mitano zaidi ambapo watu hawataweza kulima wala kuvuna mavuno. Mungu alinileta huku niwatangulie, ili kusalimisha maisha yenu mbaki hai nchini na kuwakomboa kwa ukombozi mkubwa. Kwa hiyo, si nyinyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Ndiye aliyenifanya kama baba kwa Farao, msimamizi wa nyumba yake yote na mtawala wa nchi yote ya Misri.