Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 43:24-34

Mwanzo 43:24-34 Biblia Habari Njema (BHN)

Huyo msimamizi alipowakaribisha nyumbani kwa Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu yao, na punda wao akawalisha. Nao wakatayarisha zawadi zao za kumpa Yosefu, kwa sababu walisikia kuwa watakula pamoja naye. Yosefu, aliporudi nyumbani, wakamletea zile zawadi walizokuwa nazo, wakamwinamia kwa heshima. Yosefu akawauliza habari zao na kusema, “Mlinisimulia habari za mzee, baba yenu. Je, hajambo? Angali hai?” Wakamjibu, “Mtumishi wako, baba yetu, hajambo na angali hai.” Kisha wakainama kwa heshima. Yosefu alipoinua macho yake na kumwona Benyamini, nduguye, mtoto wa mama yake, akasema, “Huyu ndiye ndugu yenu mdogo mliyeniambia habari zake? Mungu na akufadhili, mwanangu!” Ghafla, Yosefu akatoka mahali hapo, kwani machozi yalikuwa yanamlengalenga kwa shauku kubwa juu ya ndugu yake, akaingia chumbani mwake na kuangua kilio. Baada ya kunawa uso wake, alitoka huku akijikaza, akaamuru chakula kiletwe. Yosefu aliandaliwa chakula chake peke yake, na ndugu zake wakaandaliwa peke yao, hali kadhalika na Wamisri waliokula pamoja naye, wakaandaliwa peke yao, kwani ni chukizo kwa Wamisri kula chakula pamoja na Waebrania. Ndugu zake Yosefu waliketi mbele yake kulingana na umri wao, kuanzia wa kwanza hadi wa mwisho, wakawa wanaangaliana kwa mshangao. Chakula kilikuwa kikichukuliwa kutoka mezani pa Yosefu na kupelekwa kwao, lakini Benyamini alipewa mara tano zaidi ya kiasi walichopewa ndugu zake. Basi, wakanywa na kufurahi pamoja naye.

Shirikisha
Soma Mwanzo 43

Mwanzo 43:24-34 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Msimamizi akawapeleka wale watu katika nyumba ya Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu na kuwapa punda wao majani. Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yosefu wakati atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko. Yosefu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi walizokuwa nazo, ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia hadi nchi. Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?” Wakamjibu, “Mtumishi wako baba yetu bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama chini kumpa heshima. Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.” Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yosefu akatoka nje kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo. Baada ya kunawa uso wake, akatoka nje na huku akijizuia akasema, “Pakueni chakula.” Wakampakulia Yosefu peke yake, ndugu zake peke yao na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri. Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao. Wakati walipelekewa sehemu ya chakula kutoka mezani mwa Yosefu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.

Shirikisha
Soma Mwanzo 43