Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 43

43
Ndugu zake Yusufu warudi, wakimleta Benyamini
1 # Mwa 12:10; 26:1; 41:57; 1 Fal 18:2; 2 Fal 8:1; Yer 52:6 Njaa ikawa kali katika nchi. 2Ikawa walipokwisha kula nafaka waliyoileta kutoka Misri, baba yao akawaambia, Rudini huko, mkatununulie chakula kidogo. 3#Mwa 42:20; 44:23 Yuda akamwambia akisema, Yule mtu alituagizia sana akisema, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. 4Ukimtuma ndugu yetu pamoja nasi, tutashuka na kukununulia chakula. 5Ila usipomtuma, hatushuki, maana mtu yule alituambia, Hamtaniona uso wangu, ndugu yenu asipokuwa pamoja nanyi. 6Israeli akasema, Mbona mmenitendea vibaya hata mkamwarifu mtu yule ya kwamba mna ndugu mwingine? 7Wakasema, Mtu yule alituhoji sana habari zetu na za jamaa yetu, akisema, Baba yenu angali hai? Mnaye ndugu mwingine? Nasi tukamjibu sawasawa na maswali hayo. Je! Tungaliwezaje kujua ya kwamba atasema, Shukeni pamoja na ndugu yenu?
8Yuda akamwambia Israeli baba yake, Mtume kijana pamoja nami, tuondoke, tuende zetu, ili tupate kuishi, wala tusife, sisi na wewe na watoto wetu. 9#Mwa 44:32; Flm 1:18,19 Mimi nitakuwa mdhamini wake, umtake mkononi mwangu. Nisipomleta tena kwako, na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye hatia mbele yako daima; 10maana kama hatungalikawia, hakika tungaliisha kurudi mara ya pili. 11#Mwa 32:20; 37:25; Mit 18:16; Yer 8:22; Eze 27:17 Israeli, baba yao, akawaambia, Kama ndivyo, fanyeni hivi; twaeni tunu za nchi katika vyombo vyenu, mkamchukulie mtu huyo zawadi, zeri kidogo, na asali kidogo, ubani, na manemane, na jozi, na lozi. 12#Mwa 42:25,35 Mkatwae fedha maradufu mikononi mwenu, na fedha zile zilizorudishwa kinywani mwa magunia yenu zirudisheni mikononi mwenu; labda zilisahauliwa. 13Mtwaeni na ndugu yenu, mwondoke na kurudi kwa mtu yule. 14#1 Sam 14:6; 2 Sam 22:3,31; Ayu 13:15; Zab 22:4; 34:8,22; Mit 28:5; Isa 57:13; Nah 1:7 Mungu Mwenyezi na awape rehema usoni pa mtu yule ili awafungulie ndugu yenu huyo mwingine, na Benyamini. Nami nikifiwa na watoto wangu, nimefiwa.
15Basi hao watu wakatwaa zawadi ile, wakatwaa na fedha maradufu mikononi mwao, na Benyamini; wakaondoka, wakashuka mpaka Misri, wakasimama mbele ya Yusufu. 16#Mwa 24:2; 39:4 Naye Yusufu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, Uwalete watu hawa nyumbani, ukachinje mnyama na kuwaandalia, maana watu hawa watakula pamoja nami adhuhuri. 17Yule mtu akafanya kama Yusufu alivyomwambia Naye akawaleta watu hao nyumbani mwa Yusufu. 18Lakini watu hao wakaogopa kwa sababu wameletwa nyumbani mwa Yusufu, wakasema, Kwa sababu ya fedha zile zilizorudishwa katika magunia yetu mara ya kwanza tumeletwa humu; apate kutushitaki, na kutushika, atutwae sisi kuwa watumwa, na punda wetu.
19Wakamkaribia yule msimamizi wa nyumba ya Yusufu, wakasema naye mlangoni pa nyumba. 20Wakamwambia, Tazama, bwana, kweli tulishuka mara ya kwanza ili tununue chakula. 21#Mwa 42:27,35 Ikawa, tulipofika nyumba ya wageni, tukafungua magunia yetu, kumbe! Fedha za kila mtu zilikuwako kinywani mwa gunia lake, fedha zetu kwa uzani wake kamili; nasi tumezileta tena mikononi mwetu. 22Nasi tumeleta fedha nyingine mikononi mwetu ili tununue chakula; hatujui ni nani aliyezitia fedha zetu katika magunia yetu. 23Akawaambia, Amani iwe kwenu, msiogope; Mungu wenu, naye ni Mungu wa baba yenu, amewapa akiba katika magunia yenu; fedha zenu zilinifikia. Kisha akawatolea Simeoni kwao.
24 # Mwa 18:4; 24:32; Lk 7:44; Yn 13:5; 1 Tim 5:10 Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakanawa miguu, akawapa punda wao chakula. 25Wakaiweka tayari ile zawadi hadi atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko. 26#Mwa 27:29; 33:6; Rut 2:10 Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka chini. 27#Mwa 42:11-13 Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai? 28#Mwa 37:7,10; Mit 14:19 Wakasema, Mtumishi wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu. 29#Mwa 35:17,18; 42:13 Akainua macho yake, akamwona Benyamini, nduguye, mwana wa mama yake, akasema, Huyu ndiye ndugu yenu mdogo, mliyeniambia habari zake? Akasema, Mungu akufadhili, mwanangu. 30#1 Fal 3:26; Yer 31:20; Mwa 42:24; 2 Sam 18:33 Yusufu akafanya haraka, kwa sababu moyo wake ulimwonea shauku nduguye, akatafuta pa kulilia, akaingia chumbani mwake, akalilia humo.
31 # Mwa 43:25 Akanawa uso, akatoka, akajizuia, akasema, Leteni chakula. 32#Mwa 46:34; Kut 8:26 Wakamwandalia yeye peke yake, na wao peke yao, na wale Wamisri waliokula pamoja naye peke yao; maana Wamisri hawawezi kula pamoja na Waebrania, kwa kuwa ni chukizo kwa Wamisri. 33Wakaketi mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa haki ya uzawa wake, na mdogo kwa udogo wake; watu hao wakastaajabu wao kwa wao. 34#Mwa 45:22 Wakapelekewa sehemu za chakula kutoka mezani pake, lakini akazidisha sehemu ya Benyamini iwe kubwa mara tano kuliko zao. Wakanywa, wakafurahi pamoja naye.

Iliyochaguliwa sasa

Mwanzo 43: SRUV

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha