Mwa 43:24-34
Mwa 43:24-34 SUV
Mtu yule akawaleta wale watu nyumbani mwa Yusufu, akawapa maji, wakatawadha miguu, akawapa punda zao chakula. Wakaiweka tayari ile zawadi hata atakapokuja Yusufu adhuhuri, maana wamesikia ya kwamba watakula chakula huko. Alipokuja Yusufu nyumbani, wakamletea ile zawadi iliyokuwa mikononi mwao nyumbani mwake, wakamwinamia mpaka nchi. Akawaulizia hali yao, akasema, Je! Baba yenu, yule mzee mliyemnena, hajambo? Angali hai? Wakasema, Mtumwa wako baba yetu hajambo, angali hai; wakainama, wakasujudu. Akainua macho yake, akamwona Benyamini, nduguye, mwana wa mamake, akasema, Huyu ndiye ndugu yenu mdogo, mliyeniambia habari zake? Akasema, Mungu akufadhili, mwanangu. Yusufu akafanya haraka, kwa sababu moyo wake ulimwonea shauku nduguye, akatafuta pa kulia, akaingia chumbani mwake, akalia humo. Akanawa uso, akatoka, akajizuia, akasema, Leteni chakula. Wakamwandalia yeye peke yake, na wao peke yao, na wale Wamisri waliokula pamoja naye peke yao; maana Wamisri hawawezi kula pamoja na Waebrania, kwa kuwa ni chukizo kwa Wamisri. Wakaketi mbele yake, mzaliwa wa kwanza kwa cheo cha kuzaliwa kwake, na mdogo kwa udogo wake; watu hao wakastaajabu wao kwa wao. Wakapelekewa sehemu za chakula kutoka mezani pake, lakini akazidisha sehemu ya Benyamini iwe kubwa mara tano kuliko zao. Wakanywa, wakafanya furaha pamoja naye.