Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mwanzo 42:14-28

Mwanzo 42:14-28 Biblia Habari Njema (BHN)

Lakini Yosefu akawaambia, “Ni kama nilivyosema: Nyinyi ni wapelelezi tu. Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Naapa kwa jina la Farao, kwamba hamtatoka hapa mpaka mdogo wenu atakapokuja. Mtumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu mdogo, wakati wengine wenu wanamngoja gerezani. Hapo ndipo maneno yenu yatakapojulikana ukweli wake. La sivyo, naapa kwa jina la Farao kwamba nyinyi ni wapelelezi.” Kisha akawatia wote gerezani kwa muda wa siku tatu. Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Kwa kuwa mimi ni mcha Mungu, fanyeni hivi ili mpate kuishi: Kama kweli nyinyi ni watu waaminifu, mmoja wenu na abaki kifungoni, na wengine wawapelekee nafaka jamaa zenu wenye njaa. Kisha mleteni kwangu ndugu yenu mdogo. Hii itathibitisha ukweli wa maneno yenu, nanyi hamtauawa.” Basi, wakakubali kufanya hivyo. Kisha wakasemezana wao kwa wao, “Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu. Ingawa tulimwona akisononeka rohoni mwake, sisi hatukumjali hata alipotusihi. Ndiyo maana taabu hii yote inatupata.” Reubeni akawaambia, “Je, mimi sikuwaambieni tusimdhuru kijana? Lakini nyinyi hamkunisikiliza! Sasa tunaadhibiwa kwa ajili ya damu yake.” Wao hawakujua kuwa Yosefu alielewa yote hayo waliyosema, maana alipoongea nao ilikuwa kwa njia ya mkalimani. Yosefu akaenda kando, akaangua kilio. Alipotulia, akarudi kuzungumza nao. Kisha akamkamata Simeoni na kumtia pingu mbele ya macho yao. Yosefu akatoa amri mifuko yao ijazwe nafaka, kila mmoja wao arudishiwe fedha yake katika gunia lake, na wapewe chakula cha njiani. Wakafanyiwa mambo hayo yote. Wakawatwisha punda wao mizigo yao ya nafaka, wakaondoka. Ikawa walipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili apate kumlisha punda wake, akashangaa kukuta fedha yake mdomoni mwa gunia lake. Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Hii hapa mdomoni mwa gunia langu!” Waliposikia hayo, wakafa moyo. Wakatazamana huku wanatetemeka na kuulizana, “Ni jambo gani hili alilotutendea Mungu?”

Shirikisha
Soma Mwanzo 42

Mwanzo 42:14-28 Swahili Revised Union Version (SRUV)

Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi. Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo. Mtumeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa jela, hadi maneno yenu yahakikishwe kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao hakika ninyi ni wapelelezi. Akawatia wote gerezani siku tatu. Siku ya tatu, Yusufu akawaambia, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. Kama ninyi ni wa kweli, mmoja wenu na afungwe gerezani, nanyi mwende mkachukue nafaka kwa ajili ya njaa ya nyumba zenu, mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia, kwa hiyo shida hii imetupata. Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, Msimkosee kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo tunadaiwa damu yake. Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alizungumza nao kupitia kwa mkalimani. Akaenda kando, akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao. Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani. Na hivyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakawatwika punda wao nafaka yao, wakatoka huko. Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake. Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, Ni nini hii Mungu aliyotutendea?

Shirikisha
Soma Mwanzo 42

Mwanzo 42:14-28 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)

Yusufu akawaambia, Ndivyo nilivyowaambia, nikisema, Wapelelezi ninyi. Mtabainika kwa njia hii; aishivyo Farao, hamtoki hapa, asipokuja huku huyo ndugu yenu mdogo. Mpelekeni mmoja wenu, aende akamlete ndugu yenu, na ninyi mtafungwa, hata maneno yenu yahakikishwe, kama mna kweli ninyi; ikiwa sivyo, aishivyo Farao, ninyi ni wapelelezi. Akawatia wote gerezani siku tatu. Yusufu akawaambia siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. Kama ni wa kweli ninyi ndugu yenu mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mkamlete ndugu yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya. Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi, wala hatukusikia kwa hiyo shida hii imetupata. Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema, msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. Wala hawakujua ya kwamba Yusufu anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao. Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao. Yusufu akaamuru kuvijaza vyombo vyao nafaka, na kumrudishia kila mtu fedha yake katika gunia lake, na kuwapa chakula cha njiani. Navyo ndivyo walivyofanyiwa. Wakaweka nafaka yao juu ya punda zao, wakatoka huko. Mmoja wao alipofungua gunia lake ili ampe punda wake chakula katika nyumba ya wageni, aliiona fedha yake; kumbe! Iko kinywani mwa gunia lake. Akawaambia nduguze, Fedha yangu imerudishwa, angalia, imo humo guniani mwangu. Mioyo yao ikazimia, wakageukiana wakitetemeka, wakasema, N’nini hii Mungu aliyotutendea?

Shirikisha
Soma Mwanzo 42

Mwanzo 42:14-28 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)

Yosefu akawaambia, “Ni sawa kabisa kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi! Na hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa mpaka ndugu yenu mdogo aje hapa. Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu, wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!” Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu. Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu: Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa. Lakini ni lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo. Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuponya maisha yake, lakini hatukumsikiliza, hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.” Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.” Hawakujua kuwa Yosefu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani. Yosefu akajitenga nao akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akataka Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao. Yosefu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe mahitaji ya njiani. Baada ya kufanyiwa hayo yote, wakapakiza nafaka juu ya punda zao, wakaondoka. Walipofika mahali pa kulala huko njiani mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake, akakuta fedha yake kwenye mdomo wa gunia lake. Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.” Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”

Shirikisha
Soma Mwanzo 42