Mwanzo 42:14-28
Mwanzo 42:14-28 NENO
Yusufu akawaambia, “Kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi! Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa hadi ndugu yenu mdogo aje hapa. Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu. Wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!” Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu. Siku ya tatu, Yusufu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu: Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa. Lakini lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo. Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuokoa maisha yake, lakini hatukumsikiliza. Hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.” Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.” Hawakujua kuwa Yusufu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani. Yusufu akajitenga nao, akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akaamuru Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao. Yusufu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe chakula cha njiani. Baada ya kutendewa hayo yote, wakapakiza nafaka juu ya punda wao, wakaondoka. Walipofika mahali pa kulala huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake; akakuta fedha yake ndani ya gunia lake. Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.” Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”