Wagalatia 3:15-29
Wagalatia 3:15-29 Biblia Habari Njema (BHN)
Ndugu, nitawapeni mfano kutoka maisha yetu ya kila siku. Fikirini juu ya mkataba kati ya watu wawili. Mkataba ukisha fanyika na kutiwa sahihi hapana mtu anayeuweka kando au kuuongezea kitu. Basi, Abrahamu alipewa ahadi, yeye pamoja na mzawa wake. Maandiko hayasemi: “Na wazawa wake,” yaani wengi, bali yasema, “Na mzawa wake,” yaani mmoja, naye ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni hiki: Mungu alifanya agano lake, akalithibitisha; sheria ambayo ilitokea miaka 430 baadaye, haiwezi kulitangua hilo agano wala kuibatilisha hiyo ahadi. Maana, kama zawadi ya Mungu inategemea sheria, basi, haiwezi kutegemea tena ahadi ya Mungu. Kumbe, lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa sababu aliahidi. Ya nini basi, sheria? Iliongezwa hapo ili kuonesha uhalifu ni kitu gani, mpaka atakapokuja yule mzawa wa Abrahamu aliyepewa ile ahadi. Sheria ililetwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Ama hakika, mpatanishi hahitajiwi ikiwa jambo lenyewe lamhusu mtu mmoja; na Mungu ni mmoja. Je, sheria inapingana na ahadi za Mungu? Hata kidogo! Maana, kama kungalitolewa sheria ambayo ingeweza kuwapa watu uhai, basi, tungeweza kufanywa waadilifu kwa njia ya sheria. Lakini sivyo; Maandiko Matakatifu yamekwisha sema kwamba ulimwengu wote upo chini ya utawala wa dhambi; na hivyo, wenye kuamini watimiziwe ile ahadi aliyotoa Mungu, kwa kumwamini Yesu Kristo. Kabla ya kujaliwa imani, sheria ilitufanya wafungwa, tukingojea imani hiyo ifunuliwe. Basi, hiyo sheria ilikuwa kama mlezi wetu mpaka alipokuja Kristo, ili kwa njia ya imani tufanywe waadilifu mbele yake Mungu. Lakini kwa vile ile imani imekwisha fika, sisi hatuko tena chini ya mlezi. Kwa njia ya imani, nyinyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu kwa kuungana na Kristo. Nyinyi nyote mliobatizwa mkaungana na Kristo ni kama vile mmemvaa Kristo. Hivyo, hakuna tena tofauti kati ya Myahudi na Mgiriki, mtumwa na mtu huru, mwanamume na mwanamke. Nyote ni kitu kimoja kwa kuungana na Kristo Yesu. Ikiwa nyinyi ni wa Kristo, basi ni wazawa wa Abrahamu, na mtapokea yale aliyoahidi Mungu.
Wagalatia 3:15-29 Swahili Revised Union Version (SRUV)
Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno. Basi ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazawa, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Abrahamu kwa njia ya ahadi. Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hadi aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe. Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja. Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, hakika haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hakuna Myahudi wala Mgiriki. Hakuna mtumwa wala huru. Hakuna mwanamume wala mwanamke. Maana ninyi nyote mmekuwa wamoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Abrahamu, na warithi kulingana na ahadi.
Wagalatia 3:15-29 Maandiko Matakatifu ya Mungu Yaitwayo Biblia (SUV)
Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno. Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo. Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi. Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi. Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe. Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja. Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria. Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo. Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani. Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.
Wagalatia 3:15-29 Neno: Bibilia Takatifu (NEN)
Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi. Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja. Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini. Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria. Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.