Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Wagalatia 3:15-29

Wagalatia 3:15-29 NEN

Ndugu zangu, nataka nitoe mfano kutoka maisha ya kila siku. Kama vile hakuna mtu awezaye kutangua au kuongeza kitu katika agano la mtu ambalo limekwisha kuthibitishwa, vivyo hivyo kwa hali kama hii. Ahadi zilinenwa kwa Abrahamu na kwa mzao wake. Maandiko hayasemi “kwa wazao,” likimaanisha watu wengi, bali “kwa mzao wako,” yaani mtu mmoja, ndiye Kristo. Ninachotaka kusema ni kwamba, sheria, ambayo ilitolewa miaka 430 baadaye, haitangui Agano lililothibitishwa na Mungu ili kuibatilisha ahadi ile. Kwa maana kama urithi hupatikana kwa sheria, basi hautegemei tena ahadi, lakini Mungu kwa neema yake alimpa Abrahamu urithi kwa njia ya ahadi. Kwa nini basi iwepo sheria? Sheria iliwekwa kwa sababu ya makosa mpaka atakapokuja yule Mzao wa Abrahamu, ambaye alitajwa katika ile ahadi. Sheria iliamriwa na malaika kwa mkono wa mpatanishi. Basi mpatanishi huhusisha zaidi ya upande mmoja, lakini Mungu ni mmoja. Je basi, sheria inapingana na ahadi za Mungu? La hasha! Kwa maana kama sheria iliyotolewa ingeweza kuwapa watu uzima, basi haki ingepatikana kwa njia ya sheria. Lakini Maandiko yamefanya vitu vyote vifungwe chini ya nguvu ya dhambi, ili yale yaliyoahidiwa kwa njia ya imani katika Yesu Kristo yapate kupewa wale wanaoamini. Kabla imani hii haijaja tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ile imani ifunuliwe. Hivyo, sheria ilikuwa kiongozi kutufikisha kwa Kristo, ili tupate kuhesabiwa haki kwa imani. Lakini sasa kwa kuwa ile imani imekuja, hatusimamiwi tena na sheria. Kwa maana ninyi nyote mmekuwa watoto wa Mungu katika Kristo Yesu kwa njia ya imani. Kwa maana wote mliobatizwa ndani ya Kristo, mmemvaa Kristo. Wala hakuna tena Myahudi au Myunani, mtumwa au mtu huru, mwanaume wala mwanamke, maana nyote mmekuwa wamoja ndani ya Kristo Yesu. Nanyi mkiwa ni mali ya Kristo, basi ninyi ni wa uzao wa Abrahamu na warithi sawasawa na ile ahadi.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Wagalatia 3:15-29